Na mwandishi wetu
Mabao ya Clement Mzize na Maxi Nzengeli yametosha kuifanya Yanga ianze mbio za kulitetea taji la Ligi Kuu NBC kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Nzengeli ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia Yanga bao katika dakika ya 26 kwa shuti wakati bao la pili likifungwa na Mzize akiitumia pasi ya Stephane Aziz Ki dakika mbili kabla ya kutimia dakika ya 90.
Yanga hata hivyo wangeweza kupata mabao mengi zaidi kama si makosa ya washambuliaji wake Prince Dube aliyeshindwa kuzitumia vizuri nafasi tatu wakati Pacome Zouzoua naye alishindwa kuzitumia nafasi mbili kuipatia timu hiyo mabao.
Ushindi wa Yanga hata hivyo haujaweza kuiondoa Simba kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili tofauti na Yanga ambayo ndio kwanza imecheza mechi ya kwanza.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, mambo yamekuwa magumu kwa Azam ambao baada ya kuaga mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afika, leo wamejikuta wakitoka sare ya ugenini ya 0-0 mbele JKT Tanzania.
Nao Coastal Union au Wagosi wa Kaya wakiwa ugenini KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam walijikuta wakitoka sare ya bao 1-1 mbele ya KMC, bao la wenyeji KMC likifungwa na Ibrahim Elias dakika ya 33 wakati la Coastal lilifungwa na Maabad Maabad dakika ya 87.
Soka Maxi, Mzize waiadhibu Kagera
Maxi, Mzize waiadhibu Kagera
Read also
