Na mwandishi wetu
Wachezaji wawili wakongwe, Mbwana Samatta na Simon Msuva wameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kilichotangazwa Jumatatu hii na kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Wakati Msuva akiachwa kwa mara ya kwanza, hii ni mara ya pili kwa Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo kuachwa katika kikosi hicho, awali aliachwa katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia ambao Stars ilishinda kwa bao 1-0.
Mbali na wachezaji hao, Morocco pia amemuacha katika kikosi hicho kipa wa Simba, Aishi Manula na badala yake amewaita Ally Salim wa Simba, Aboutwalib Mshery wa Yanga na Yona Amos wa Pamba ya Mwanza.
Kikosi hicho cha Stars kitajinoa kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambapo timu hiyo ipo Kundi H pamoja na timu za DR Congo, Ethiopia na Guinea.
Wachezaji wengine walioitwa na Morocco katika kikosi hicho ni Mohammed Hussein, Nathaniel Chilambo, Lusajo Mwaikenda, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad Bacca, Pascal Msindo na Dickson Kibabage.
Wengine ni Adolf Mtasigwa, Abdulmalick Zakaria, Himid Mao, Mudathir Yahya, Novatus Dismas, Edwin Balua, Hussein Semfukwe, Feisal Salum, Wazuri Junior, Abel Josiah, Cyprian Kachwele na Clement Mzize.
Stars itazianza mbio za Afcon 2025 Septemba 2 kwa kuumana na Ethiopia kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na katika mechi inayofuata ambayo itapigwa Septemba 10, timu hiyo itakuwa ugenini dhidi ya Guinea.
Kimataifa Samatta aachwa tena Stars
Samatta aachwa tena Stars
Read also
