London, England
Joao Mendes ambaye ni mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Barcelona, Ronaldinho yuko katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kujiunga na klabu ya Burnley ya England.
Kocha wa Burnely, Scott Parker alithibitisha kuwa klabu hiyo ipo katika mpango wa kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ingawa haitaki suala hilo kuwa gumzo kubwa kwenye vyombo vya habari.
Mendes ambaye amekuwa katika akademi ya Barcelona, anatarajia kuwajili Burnley wakati wowote kuanzia sasa baada ya taratibu za awali kukamilika.
Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo atasaini mkataba wa miaka miwili na Parker amekiri kwamba kumekuwa na mazungumzo ya karibu baina ya pande mbili husika.
“Hakuna ambacho kimekamilika rasmi kwa wakati huu, ni kweli kwamba kuna jambo linaloendelea, tunamuona kuwa ni mchezaji anayeweza kuwa na maendeleo na anaweza kuwa sahihi lakini kuna mambo ya kusaini mikataba ambayo hayajakamilika,” alisema Parker.
Parker alisema kwamba anavutiwa na jambo hilo kutokana na sifa za baba wa mtoto huyo lakini anadhani haitokuwa sahihi kulifanya jambo hilo kubwa na kumuweka katika hali ya presha mchezaji huyo kwa kuwa nimchezaji ni mwenye kujiunga na timu ili kuendeleza kipaji chake.
Awali Mendes alianza kucheza soka Brazil kabla ya kuhamia katika akademi ya Barcelona mwaka 2023 na kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya vijana chini ya miaka 19 cha timu hiyo.
Burnley ambayo imewahi kucheza Ligi Kuu England kwa sasa ini timu inayoshiriki Ligi ya Championship.
Ronaldinho au Gaucho ni mmoja wa wachezaji waliokuwa tishio akitamba katika klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Brazil.
