Paris, Ufaransa
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Thomas Bach (pichani) amepanga kuondoka kwenye nafasi hiyo mwakani akidai kwamba harakati za Olimpiki zitaweza kwenda vizuri kukiwa na mabadiliko ya uongozi.
Bach amekuwa kiongozi IOC tangu Septemba 2013 na hivyo kuongoza kwa miaka takriban 12 hadi sasa na uongozi wake unafikia ukomo mwakani.
Utaratibu wa viongozi kuwa madarakani kwa muda maalum uliwekwa kwa lengo la kudhibiti vitendo vya rushwa takriban miaka 25 iliyopita baada ya kashfa ya Salt Lake City iliyohusisha kuwania uenyeji wa Michezo ya Olimpki.
Uvumi ulianza kuibuka takriban mwaka mmoja uliopita kwamba Bach huenda angeendelea kubaki katika ofisi yake baada ya wajumbe kumtaka abadili kanuni ya Olimpiki ambayo itaufanya uongozi wake uwe na ukomo.
Bach, 70, hata hivyo alizima uvumi huo Jumamosi hii akiwa jijini Paris kwenye Michezo ya Olimpiki aliposema kwamba IOC inahitaji kiongozi mpya wa kuendeleza harakati za Olimpiki katika dunia yenye changamoto za kidigitali na kisiasa.
“Nyakati mpya zinahitaji viongozi wapya, mimi kwa umri wangu si nahodha sahihi, najua kwa uamuzi huu nitakuwa nimewakatisha tamaa wengi wenu,” alisema Bach.
Uchaguzi wa IOC unatarajia kufanyika katika mkutano wa wanachama Machi mwakani nchini Ugiriki na tayari jina la makamu rais wa IOC, Juan Antonio Samaranch ambaye pia ni mtoto wa rais wa zamani wa IOC limekuwa likitajwa.
Baba yake Juan aliongoza IOC kwa miaka 21 kabla ya kung’atuka mwaka 2001 baada ya vuguvugu la kashfa ya Salt Lake na haitoshangaza mtoto wake akichukua nafasi hiyo iliyowahi kushikwa na baba yake.
Mwingine ni Nicole Hoevertsz ambaye pia ni makamu rais IOC, pia yamo majina ya Mwanamfalme wa Jordan, Feisal Al Hussein na bingwa wa zamani wa Olimpiki kwenye mashindano ya kuogelea, Kirsty Coventry kutoka Zimbabwe ambao wote ni wajumbe wa bodi ya IOC.
Jina lingine linalotajwa katika mbio za kumrithi Bach ni la Sebastian Coe, bingwa wa zamani mara mbili wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500. Coe pia alikuwa kiongozi katika kamati ya Michezo ya Olimpiki ya London 2012.
Coe pamoja na sifa zote anazohusishwa nazo ikiwamo kuwa mjumbe katika baraza la kutunga sheria nchini Uingereza, umri wake wa miaka 68 unaweza kumuweka pagumu kupitishwa kuongoza IOC.
Kimataifa Rais IOC atangaza kung’atuka
Rais IOC atangaza kung’atuka
Read also
