Na mwandishi wetu
Yanga imeibugiza Azam FC mabao 4-1 na kubeba Ngao ya Jamii katika mechi iliyopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Azam ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 13, mfungaji akiwa nyota wa zamani wa Yanga, Fei Toto akiitumia vyema pasi ya chinichini iliyopigwa na Jirbil Sillah na Blanco kuupisha mpira kabla ya kumkuta mfungaji.
Bao hilo lilikuwa kama limewachochea moto Yanga ambao waliandika bao la kwanza dakika tano baadaye mfungaji akiwa ni Prince Dube aliyeinasa pasi ya Mudathir Yahya na kumzidi ujanja YanickBangala ambaye alijaribu kumzuia bila mafanikio.
Azam ambao walionekana kama kuchanganyikiwa waliizawadia Yanga bao dakika ya 27 baada ya Yoro Diaby kujifunga wakati akiokoa krosi iliyochongwa na Shadrack Boka.
Dakika tatu baadaye mambo yaliwaharibikia Azam waliojikuta wakichapwa bao la tatu mfungaji akiwa Stephane Aziz Ki, mpira uliotokana na shambulizi la Pacome ambaye shuti lake liliokolewa na kipa wa Azam Mohammed Mustapha.
Baada ya Mustapha kuokoa mpira huo, Diaby aliutoa na kuwa kona ambayo Yanga walipiga kona fupi na Aziz Ki kuitumia vyema kufumua shuti lililombabatiza Bangala na kumchanganya kipa kabla ya kujaa wavuni.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihitimishwa na Clement Mzize ambaye aliinasa pasi ya Clatous Chama katika dakika ya 90 na kufumua shuti la chinichini lililomshinda kipa wa Azam na kujaa wavuni.
Katika mechi hiyo timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji Yanga ikiwatoa Dube, Mudathir, Aziz Ki, Pacome na Aucho na kuwaingiza Mzize, Mwamnyeto, Chama, Musonda na Aziz Andambwile wakati Azam iliwatoa Akaminko, Sidibe na nafasi zao kuchukuliwa na Eva Merza na Adam Adam.
Katika mechi ya kuska mshindi wa tatu iliyopigwa kabla ya mechi ya Yanga na Azam, Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Soka Yanga yaibugiza Azam 4-1, yabeba Ngao ya Jamii
Yanga yaibugiza Azam 4-1, yabeba Ngao ya Jamii
Read also
