Na mwandishi wetu
Yanga imeifanya siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi kuwa tamu baada ya kuifumua Red Arrows ya Zambia mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Jumapili hii Agosti 4, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kama ilivyo ada Kilele cha Wiki ya Mwananchi imekwenda sambamba na tamasha ambalo lilianza asubuhi likihusisha matukio mbalimbali ya kijamii, burudani ya muziki, utambulisho wa wachezaji kabla ya kuhitimishwa kwa mechi hiyo.
Wakishangiliwa na mashabiki lukuki walioujaza vyema Uwanja wa Mkapa na jezi zao za rangi ya kijani na njano, Yanga walishtushwa dakika ya sita tu ya mchezo huo baada ya Arrows kuandika bao lililofungwa na Ricky Banda.
Bao hilo la mapema lililotokana na makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga kushindwa kujipanga na hivyo kumpa nafasi Banda kuruka na kuujaza wavuni mpira kwa kichwa mbele ya kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwanyamazisha mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia timu yao mwanzo mwisho lakini ghafla wakawa kama vile wameingiwa na hofu ya kupoteza mchezo huo.
Kipindi cha pili kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji wake wakati huo Arrows wakionekana kama wenye kujihami zaidi na Yanga kushindwa kuzitumia nafasi kadhaa walizotengeneza.
Yanga walianza kuhesabu bao lao la kwanza katika dakika ya 64 mfungaji akiwa ni Mudathir Yahya, aliyeujaza mpira wavuni kwa mguu wa kushoto akiwa nje kidogo ya eneo la penalti.
Bao hilo lilionekana kuipa nguvu zaidi Yanga huku Arrows ambao pia ni mabingwa wa Kombe la Kagame, wakipambana kujihami na kufanya mashambulizi machache hali iliyoufanya mchezo huo kuwa mzuri na uliojaa ushindani kwa timu zote.
Alikuwa ni Stephane Aziz Ki aliyewainua vitini mashabiki wa Yanga kwa bao la penalti iliyotolewa katika dakika ya 90 baada ya Nickson Kibabage kuchezewa rafu katika eneo la penalti na hatimaye kuifanya Siku ya Mwananchi iwe tamu.
Mgeni rasmi katika mechi hiyo na kilele cha Wiki ya Mwananchi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango ambaye pia anaaminika kuwa ni shabiki wa timu ya Yanga.
Kimataifa Yanga yaifumua Red Arrows 2-1
Yanga yaifumua Red Arrows 2-1
Read also
