Bordeaux, Ufaransa
Ufaransa itaumana na Misri katika nusu fainali ya soka kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris baada ya kuibwaga Argentina bao 1-0, mechi iliyoandamana na matukio ya vurugu mara baada ya dakika 90 kukamilika.
Baada ya mwamuzi kumaliza mchezo, wachezaji na makocha wa Ufaransa na Argentina waliingia katika mzozo ndani ya uwanja hali ambayo haikuleta picha nzuri licha ya wenyeji kufurahia matokeo ya mechi hiyo.
Mshambuliaji wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta ndiye aliyepeleka kilio Argentina baada ya kuujaza wavuni mpira kwa kichwa akiitumia kona ya Michael Olise katika dakika ya tano.
Mechi hiyo pia iliandamana na matukio yaliyoashiria ubaguzi wa rangi baada ya picha za video kuwaonesha wachezaji wa Argentina wakiimba nyimbo za kuwadhihaki wachezaji wenye asili ya Afrika katika kikosi cha Ufaransa.
Sambamba na tukio hilo pia kulikuwa na tukio la zomeazomea kutoka kwa mashabiki wa Ufaaransa wakati wimbo wa taifa wa Argentina ukiimbwa kabla ya kuanza kwa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nouveau.
Ufaransa ambao mara ya mwisho kutwaa medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki ilikuwa mwaka 1984, baada ya kuitoa Argentina wataumana na Misri ambao katika mechi nyingine ya robo fainali waliilaza Paraguay kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1.
Argentina waliotwaa Kombe la Dunia mwaka 2022 baada ya kuilaza Ufaransa kwenye penalti, walitarajiwa kuendeleza wimbi la ushindi na kuweka rekodi ya kubeba mataji mfululizo kuanzia Kombe la Dunia, Copa America ambalo wamebabe hivi karibuni pamoja na kuibuka kinara katika Michezo ya Olimpiki.
Ndoto za kuweka rekodi hiyo sasa zimezimwa na timu hiyo imebaki na mataji yake mawili ya kujivunia ya Kombe la Dunia na Copa America.
Katika nusu fainali nyingine, Hispania ambao wametoka kubeba Kombe la Euro 2024, wataumana na Morocco ambapo mshindi wa mechi hiyo atakabiliana na mshindi wa mechi kati Ufaransa na Misri ili kumpata mshindi wa dunia kwenye soka katika Michezo ya Olimpiki.
Kimataifa Vurugu zatawala Ufaransa ikiibwaga Argentina kwenye Olimpiki
Vurugu zatawala Ufaransa ikiibwaga Argentina kwenye Olimpiki
Read also
