Na mwandishi wetu
Simba Day, leo Jumamosi Agosti 3, 2024 imekuwa tamu kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kuichapa APR ya Rwanda mabao 2-0 huku mashabiki wakijivunia kuujaza Uwanja wa Mkapa unaochukua mashabiki zaidi ya 60,000.
Mechi hiyo ilikuwa maalum kwa timu hiyo kujiandaa na msimu mpya wa 2024-25, ilitanguliwa na matukio mbalimbali yakiwamo ya kijamii kabla ya kufanyika utambulisho wa wachezaji wapya wa timu hiyo na wale wa zamani.
Simba au Mnyama ilikianza kipindi cha kwanza bila kuonesha kasi yoyote, iliandika bao lake la kwanza dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili, mfungaji akiwa ni nyota wake mpya Deborah Fernandes.
APR hawakuonesha kushtushwa na bao hilo waliendelea kucheza soka lao la kawaida kabla ya kujikuta wakifungwa bao la pili dakika 20 baadaye mfungaji akiwa ni Edwin Balua.
Ukiacha mabao hayo, kipindi cha kwanza kilionekana kuwa kigumu kwa timu zote ambapo Simba haikuonesha uhai kama walivyo APR ingawa kulikuwa na kosakosa za hapa na pale.
Katika kosakosa hizo, dakika ya 37, Farbrice Ngoma alimuunganishia pasi ndefu beki Mohammed Hussein ‘Zimbwe Junior’ ambaye akiwa aliumiliki mpira huo vizuri na kufanikiwa kuzalisha kona ambayo haikuwa na madhara kwa APR.
APR nao walifanya shambulizi dakika moja kabla ya mapumziko ambapo Nyibizi Ramadhan akiwa anaelekea kwenye lango la Simba alichezewa rafu na Ngoma na mwamuzi kuamuru upigwe mpira wa adhabu ambao mpigaji, Saydou Dauda alipiga shuti lililopaa juu ya lango.
Simba hata hivyo itabidi wajilaumu kwa kushindwa kupata bao la penalti iliyotolewa dakika ya 42 baada ya Joshua Mutale kuangushwa ndani ya eneo la 18 wakati akielekea kuonana na kipa wa APR, Piere Inshimwe.
Mpigaji wa penalti hiyo, Stephen Mukwale licha ya kumchambua vyema kipa wa APR ambaye aliruka upande wake wa kulia, shuti la Mukwale hata hivyo lilikwenda upande wa kushoto wa kipa huyo na kugonga mwamba.
Kocha wa Simba, Fadllu Daud aliitumia vyema mechi hiyo kuwapima wachezaji wake kwa namna ambavyo alifanya mabadiliko ya wachezaji ikiwamo kuwapa nafasi makipa watatu.
Alianza na Ally Salim ambaye baadaye aliumia na kumpisha Mussa Camara ambaye naye baadaye alitolewa na kumpisha Hussein Abel.
Simba Jumamosi ijayo itaumana na mahasimu wao Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii ambapo kocha wa Simba akiizungumzia mechi hiyo pamoja na mambo mengine alisema jambo kubwa ni suala la kujiandaa kiakili.
Kimataifa Simba Day tamu, Mnyama ampiga APR 2-0
Simba Day tamu, Mnyama ampiga APR 2-0
Read also