Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-24 wakati kiungo wa Azam Feisal Salum au Fei Toto akiibuka mchezaji bora Kombe la Shirikisho CRDB.
Wachezaji hao walitangazwa usiku wa kuamkia Ijumaa ya Agosti 2, 2024 katika hafla ya tuzo hizo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka, serikali na wadau wa michezo nchini Tanzania.
Kwa upande wa wanawake tuzo ya mchezaji bora Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) ilikwenda kwa Aisha Mnunka wakati kwenye First League aliyeshinda tuzo hiyo ni Ayoub Masoud.
Aziz Ki mbali na kutwaa tuzo ya mchezaji bora lakini pia ndiye aliyetwaa tuzo ya mfungaji bora na kiungo bora na kuwa sehemu ya wachezaji wa Yanga waliofanikiwa kubeba tuzo akiwamo kipa namba moja wa timu hiyo Djigui Diarra aliyetwaa tuzo ya kipa bora wa Kombe la Shirikisho CRDB.

Diarra hata hivyo alishindwa kutamba katika tuzo ya kipa bora Ligi Kuu NBC ambayo ilikwenda kwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi wakati kwa wanawake tuzo ya kipa bora wa TWPL ilikwenda kwa Caroline Rufo.
Beki wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Ibrahim Bacca yeye alitwaa tuzo ya beki bora wa Ligi Kuu NBC wakati mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize akibeba tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho CRDB.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi yeye amefanikiwa kutwaa tuzo ya kocha bora wakati kocha wa timu ya wanawake ya Simba, Juma Mgunda amebeba tuzo kama hiyo katika TWPL.
Nahodha wa Taifa Stars na mshambuliaji wa klabu ya Paok ya Ugiriki ambaye kwa sasa anacheza soka Saudi Arabia, Mbwana Samatta ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa Tanzania anayecheza soka nje ya Tanzania.

Kwa upande wa wanawake tuzo hiyo imekwenda kwa Aisha Masaka ambaye ni hivi karibuni tu amejiunga na klabu ya wanawake ya Brighton inayoshiriki Ligi Kuu England akitokea klabu ya DK Hacken ya Sweden.
Katika soka la ufukweni tuzo ya mchezaji bora ilikwenda kwa Jarufu Juma wakati tuzo ya mchezaji bora chipukizi ilichukuliwa na Shomari Rahim wakati kwa wanawake tuzo hiyo ilibebwa na Ester Maseke.
Ahmed Arajiga ameondoka na tuzo ya mwamuzi bora Ligi Kuu NBC, tuzo ambayo pia imebebwa na Amina Kyando katika TWPL huku kwa upande wa waamuzi wasaidizi katika Ligi Kuu NBC tuzo hiyo imebebwa na Mohamed Mkono wakati Zawadi Yusuph akibeba tuzo hiyo hiyo katika TWPL.
Wengine waliobeba tuzo ni rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga (tuzo ya heshima), Juma Bomba (tuzo ya heshima soka la wanawake) na marehemu Said El Maamry (tuzo ya Rais TFF).
Wakati huo huo timu za Mtibwa Sugar imeibuka timu yenye nidhamu kwenye Ligi Kuu NBC, tuzo ambayo pia imekwenda kwa Bunda Queens kwa upande wa TWPL.