Na mwandishi wetu
Yanga imeanza vibaya mechi za kujipima nguvu kwa kuchapwa mabao 2-1 na FC Augsburg ya Ujerumani, mechi iliyopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mbombela, Mpumalanga, Afrika Kusini.
Ikicheza soka la kuvutia lililochagizwa na mabadiliko ya kikosi cha timu hiyo yaliyofanywa mara kwa mara na kocha Miguel Gamondi, Yanga hata hivyo ilijikuta ikichapwa bao dakika ya 27 lililofungwa na Mads Pedersen.
Juhudi za Yanga ikiwa na kiungo wao mpya waliomsajili kutoka Simba, Clatous Chama hazikuweza kufua dafu mbele ya Augsburg na hadi timu zinakwenda mapumziko Yanga walikuwa nyuma kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili Yanga iliendelea na kasi ya kusaka bao la kusawazisha, Chama akishirikiana na Stephanie Aziz Ki, Mudathir Yahya, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Maxi Nzengeli hawakuweza kufua dafu mbele ya Augsburg.
Zikiwa zimebakia dakika 10 kabla ya mpira kumalizika, Augsburg, timu inayoshiriki Ligi ya Bundesliga nchini Ujerumani ilipata bao la pili lililofungwa na Phillip Tietz.
Yanga ilipambana na kupata bao lao pekee dakika sita baadaye mfungaji akiwa straika mpya wa timu hiyo, Jean Baleke ambaye aliitumia vizuri pasi ya Maxi Nzengeli.
Ukiacha Chama na Baleke, Gamondi pia katika mechi hiyo alimpa nafasi mshambuliaji mwingine mpya wa timu hiyo, Prince Dube aliyejiunga na timu hiyo akitokea Azam FC lakini hakuweza kuwa tishio mbele ya Augsburg.
Baada ya mechi ya leo, Yanga itajitupa tena uwanjani Jumatano ijayo dhidi ya TS Galaxy na baada ya hapo Julai 28 itacheza na Kaizer Chiefs katika mechi ya Kombe la Toyota.
Kimataifa Augsburg yaiadhibu Yanga 2-1
Augsburg yaiadhibu Yanga 2-1
Read also