Madrid, Hispania
Julai 16, 2024, Real Madrid inamtambulisha rasmi mshambuliaji wake mpya, Kylian Mbappe ambaye anaongeza nguvu mpya na ya kipekee katika kikosi cha timu hiyo kwenye safu ya ushambuliaji
Safu ya ushambuliaji ya Real Madrid yenye Jude Bellingham na Vinicius Junior tayari imeonesha kiwango cha juu msimu uliopita wa 2023-24 hadi kubeba taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa sasa safu hiyo imeongezewa nguvu kwa usajili wa Mbappe, mshambuliaji tishio duniani ambaye amethibitisha hilo kwenye kikosi cha PSG na timu ya taifa ya Ufaransa.
Mbio za Real Madrid kuisaka saini ya Mbappe ni za muda mrefu ingawa bila Mbappe timu hiyo imeendelea kuwa tishio na hapo unaweza kujiuliza itakuwaje timu hiyo ikiwa na Mbappe.
Itakuwaje timu hiyo ikiwa na mshambuliaji anayeshika rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika klabu ya PSG na ambaye kukosekana kwake kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Ufaransa kuliibua sintofahamu wakati wa fainali za Euro 2024.
Juhudi za kuinasa saini ya Mbappe ziliposhindwa kuzaa matunda kabla ya msimu wa 2023-24, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alisema kwamba timu yake ilikuwa imekamilika bila ya Mbappe.
Kwa Ancelloti kilichoonekana ni kwamba Mbappe hakuwa mchezaji wa kumsumbua kichwa na akalithibitisha hilo kwa kuiwezesha Real Madrid kubeba taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kauli ya Ancelloti kutoonekana mwenye kusumbuliwa na usajili wa Mbappe pia ilitoa dalili kwamba huenda mchezaji huyo asingesajiliwa Real Madrid kwa kuwa kocha aliamini maisha bila ya mchezaji huyo yanawezekana.
Ukimuweka kando Mbappe, Real Madrid ina watu wengine hatari katika safu hiyo kuanzia kwa Vinicius, Bellingham lakini hapo hapo yupo mshambuliaji wa Kibrazil, Endrick anayesubiriwa kukamilisha usajili.

Orodha hiyo pia ina Arda Guller ambaye ameonesha umahiri wake akiwa na timu ya taifa ya Uturuki kwenye fainali za Euro 2024 naye huenda akapata nafasi ya ndani ya kikosi cha Real Madrid.
Hapo hapo ikumbukwe kwamba Rodrygo naye ni mchezaji mwingine ambaye tayari ameonesha uwezo na bila shaka ana nafasi yake zaidi kwenye kikosi cha timu hiyo katika msimu wa 2024-25 pengine kuliko ilivyokuwa katika msimu ulioisha wa 2023-24.
Kwa wanaojua utamaduni wa Real Madrid, ujio wa Mbappe na mastaa wengine hauwashangazi, ni mwendelezo wa mfumo wa klabu hiyo kusajili wachezaji mastaa wakubwa wa bei mbaya au madogo wenye vipaji vya juu.
Ilikuwa hivyo tangu zama za kina Zinedine Zidane, Luis Figo, David Beckham, Ronaldo de Lima, Roberto Carlos, Kaka, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na sasa Bellingham, Vinicius Jr na hatimaye Mbappe huku Erling Haaland naye akisubiriwa.
Kwa haraka haraka unaweza kusema kwamba Real Madrid hii yenye Mbappe, Bellingham, Vinicius Jr na wengineo itashinda kila taji lililo mbele yake lakini ukweli wa mchezo wa soka hauko hivyo.
Kutafuta mfumo wa kuwatumia wachezaji hao ni jambo la kwanza gumu ambalo linaweza kumpa tabu Ancelotti kwani kuna wachezaji ambao panga pangua ni lazima wapangwe kwenye kikosi cha kwanza, ikitokea hawajapangwa kunakuwa na tatizo la ndani na wakati mwingine hata nje ya uwanja.
Kazi ngumu nyingine ngumu kwa Ancelotti ni kuwaongoza mastaa hao wa bei mbaya na kutowapa nafasi ya kumpanda kichwani na wachezaji hao kumpa hadhi na nafasi yake ya ukocha, tofauti na hivyo atajikuta pagumu.
Kazi hii ya kuwasimamia mastaa wa bei mbaya ilimshinda Jose Antonio Camacho akiwa kocha wa Real Madrid yenye Zidane, Beckham, Roberto Carlos, Ronaldo de Lima na wengineo, aliamua kujiuzulu na kueleza wazi kuwa ameshindwa kuwaongoza mastaa hao wa bei mbaya.
Tusishangae katikati ya safari ya Real Madrid hii badala ya mataji likatokea jambo kama hilo kwa Ancelotti naye akajikuta akilazimika kujiuzulu.
Sambamba na hilo pia tushishangae katikati ya safari hii tukasikia, Florentino Perez, rais wa Real Madrid amechukua uamuzi mgumu wa kumfuta kazi Ancelotti baada ya kuona mambo yanakwenda kinyume na matarajio yake.
