London, England
Klabu ya Brighton Albion ya England imetangaza kumsajili mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, Aisha Masaka kutoka klabu ya DK Hacken ya Sweden.
Taarifa ya klabu hiyo iliyopatikana Alhamisi hii haikuweka wazi undani wa mkataba wa usajili huo lakini ilibainisha kuwa mambo yote kuhusu mchezaji huyo yatategemeana na maendeleo ya soka lake.
“Tuna furaha kumkaribisha Aisha katika klabu ya Brighton, amekuwa akipambana kwa kiwango ha juu nchini Sweden na ameiwakilisha Hacken katika Ligi ya Mabingwa,” alisema Zoe Johnson, mkurugenzi mkuu wa soka la wanawake katika klabu ya Brighton.
Johnson alimtaja Aisha kuwa ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kumiliki mpira na kiasili ni mpachika mabao na wanampokea wakisubiri kumuona katika msimu mpya wa 2024-25.
Aisha, 20, mchezaji wa zamani wa timu ya Alliance ya Mwanza, mwaka 2022 alikuwa gumzo nchini Tanzania baada ya kusajiliwa na klabu ya Hacken ya nchini Sweden akitokea Yanga.
Nyota ya Aisha ilianza kung’ara katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu wa 2021 ambapo aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao 35 katika mechi 20 alizoichezea Yanga.

Katika misimu miwili na Hacken, Aisha aliisaidia timu hiyo kumaliza ligi ya wanawake Sweden kwa kushika nafasi ya pili msimu uliopita na kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya waliishia robo fainali baada ya kutolewa na PSG ya Ufaransa.
Aisha pia amewahi kuiwakilisha timu ya wanawake chini ya miaka 17 ya Tanzania na kwa Twiga Stars hadi sasa ameifungia mabao tisa katika mechi 15 tangu aanze kuichezea timu hiyo mwaka 2021.
Twiga Stars pia ikiwa na Aisha imefuzu kushiriki fainali za soka la wanawake Afrika (Wafcon) ambazo zinatarajia kufanyika mwakani nchini Morocco.