Na mwandishi wetu
Simba SC inaendelea kujitafuta, kujipanga kwa ajili ya kuonesha umwamba wake msimu ujao baada ya kushindwa kutamba katika misimu mitatu iliyopita huku mahasimu wao, Yanga SC wakitawala.
Katika kipindi ambacho Simba imeanguka baada ya utawala wa misimu yao minne ya kutwaa taji la ligi kuu, Yanga imeng’ara vya kutosha kwa kuchukua taji la ligi kuu, kufika hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika na ubingwa Kombe la FA.
Kujitutumua kwa Yanga na uwekezaji wa Azam FC iliyomaliza nafasi ya pili, yote hayo yameifanya Simba ionekane imepiga hatua mbili nyuma kwa uchambuzi wa juu juu.
Hilo limepelekea huzuni, kukosa amani na kikubwa ni lawama za mashabiki, wanachama na wapenzi kwa klabu yao. Takriban msimu mzima wa 2023-24 umekuwa wa lawama na kunyoosheana vidole na pengine hilo linachangia kwa kiasi kikubwa kuitafuna timu hiyo.
Yafuatayo ni baadhi yanayotajwa na kulalamikiwa kuidhoofisha timu hiyo ingawa hayana ushahidi wa moja kwa moja kama kweli ndiyo matatizo makubwa yanayowasumbua Wekundu hao na pengine yanatumika kuziba makosa halali yanayoivuruga Simba:
Aishi Manula
Miongoni mwa yanayoitesa Simba ni kufungwa nje ndani na Yanga msimu huu. Mechi ya kwanza ilikuwa mabao 5-1 na ya pili iliisha kwa mabao 2-1.
Matokeo ya 5-1 yaliwaumiza sana Simba na siku hiyo langoni alikuwa Aishi Manula, na ndiyo kwanza alikuwa ametoka kwenye majeraha ya muda mrefu lakini ukongwe na uzoefu wa mechi za watani ukamrejesha langoni siku hiyo.

Imani kubwa ilikuwa juu yake dhidi ya Ally Salim lakini baada ya mechi Manula alionekana hafai. Umahiri wake kwenye michuano ya klabu Afrika na kuipeleka Simba robo fainali mara nne mfululizo ulisahaulika.
Hata jina lake la utani la ‘Air Manula’ halikuvuma tena kama awali na usajili wa Ayoub Lakred kutoka FAR Rabat ukafifisha jumla jina lake na sasa mashabiki wa Simba wako tayari kipa huyo arejee Azam na wao waendelee na maisha mengine wakidai ‘ameshamaliza’!
Makosa ya timu au kuzidiwa kimbinu ndani ya dakika 90 yameshindwa kuvumilika na lawama akabebeshwa Manula ili watu nyoyo zao zipoe lakini nyuma ya pazia kipaji na umuhimu wa Manula kwa Simba na taifa zima unapotezwa kwa makusudi kwa ajili ya amani ya watu wachache na mwisho ni kama vile timu inabomolewa kupitia mlango wa nyuma.
Mangungu
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amekuwa akipokea lawama nyingi kwamba kufanya vibaya kwa timu hiyo kunachagizwa na yeye kwa madai hana mipango ya soka, yaani si mtu wa mpira.
Alipokea lawama za kutosha wakati wa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, kwani mfumo wa Robertinho ulionekana kuwakwaza licha ya kutofanya vibaya kimatokeo na Mangungu alionekana hachukui hatua kwa timu kutoridhisha.
Kipindi hiki cha usajili, hakuna anayeonekana kuamini kinachoendelea kwa hoja kwamba wachezaji wazuri Mangungu huishia kuzungumza nao tu, tofauti na wale wanaosajiliwa.
Hapa inaguswa hoja ya mshambuliaji mahiri wa Afrika ya Kati, Cesar Manzoki alipokuja Januari, mwaka jana kwenye mkutano wa Simba na kuwarushia vijembe Yanga ikionekana muda wowote nyota huyo atatua Msimbazi lakini haikuwa hivyo na mwishowe imebaki kama wimbo wa ‘kumnanga’ Mangungu.
Mashabiki wengi wa Simba wanaonekana kukosa imani na Mangungu lakini hoja zao ni kama vile hazina nguvu ya kutosha kuthibitisha hilo na badala yake ni kama wanalaumiana bila ya kujadili kinachowaangusha.
Chama
Kiungo Clatous Chama baada ya wiki iliyopita kutangazwa amehamia Yanga, baadhi ya wanazi wa Simba wameona afadhali wakiamini mchezaji huyo alikuwa ni miongoni mwa wanaowachelewesha kuisuka timu yao ya ahadi.
Inafahamika Chama amedumu Simba kwa miaka sita na uwepo wake ulionekana kama vile Simba imeridhika na ufundi mkubwa wa Mzambia huyo, inashindwa kutafuta wachezaji wa juu yake.
Lakini cha kushangaza wakati wa fununu za Chama kuelekea Jangwani, mashabiki wengi hawakupendezewa na taarifa hizo, waliona kama wananyang’anywa tonge mdomoni tena wakiwa kwenye wakati mgumu.

Ila sasa wapo wanaoona bora ameondoka ili waanze upya kuliko kuendelea kuhisi kulemaa na mchezaji mmoja ambaye aliibua tafrani msimu wa 2021-22 alipohamia RS Berkane ikionekana Simba imekosa injini ya uhakika mpaka aliporejea msimu uliofuata.
Mfungaji bora
Saido Ntibazonkiza ndiye mfungaji bora wa Simba kwa misimu miwili mfululizo. Msimu uliomalizika alifunga mabao 10 lakini bado alionekana ana mapungufu mengi, umri umeenda na sio msaada mkubwa kwa Simba, mwisho amepewa ‘thank you’.

Inafikirisha kidogo mfungaji bora wa misimu miwili mfululizo aonekane hana jambo, anaichelewesha timu lakini ndio ameshaondoka na Simba sasa inaanza upya kutafuta mpachikaji mabao mpya wa timu kuelekea msimu ujao.
Bodi ya Wakurugenzi
Kuna wakati ilielezwa Simba haina makali kwa sababu mwekezaji wao, Mohammed Dewji au Mo Dewji ameitenga bodi. Wengine wakasema kuna ‘janja-janja’ nyingi ndani ya bodi katika usajili na ndiyo maana Mo ameamua kutulia kwanza.
Mwisho wa msimu wajumbe wa bodi wanaomuwakilisha mwekezaji wameng’atuka na timu ikarejea kwa Mo mwenyewe ambaye ameweka wazi kuwa amerejea kuijenga timu hiyo kwa kishindo lakini usajili wa wachezaji wanaotua hapo mpaka sasa wanaonekana si wa hadhi ya Mo!
Mambo yamezidi kuwa mengi na siku zinazidi kuyoyoma kuelekea kuanza kwa msimu mpya, yawezekana tukaendelea kushuhudia lawama tena msimu ujao badala ya hoja za kujenga timu kwani mpaka sasa haijajulikana lishikwe lipi liachwe lipi ili timu irudi relini.
