Miami, Marekani
Argentina wana kila sababu ya kujivunia soka lao, baada ya Kombe la Dunia 2022, wamebeba taji la Copa America kwa kuilaza Colombia bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili hii.
Mechi hiyo ya fainali ililazimika kuchelewa kuanza kutokana na vurugu za nje ya uwanja na baadaye kuchezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kushindwa kumpata mshindi.
Alikuwa ni Lautaro Martinez aliyefunga bao pekee la Argentina katika dakika ya 112 akiitumia pasi ya Giovani lo Celso na hivyo kuiwezesha timu hiyo kubeba taji la Copa America kwa mara ya 16.
Mechi hiyo hata hivyo ilikuwa ngumu kidogo kwa nahodha wa Argentina, Lionel Messi ambaye alijikuta akitokwa machozi alipotolewa kipindi cha pili baada ya kuumia wakati akiwania mpira.
Majeraha haya hata hivyo hayakumzuia Messi kufurahia ushindi wa taji hilo kwa Argentina mara baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Vurugu zilizotokea nje ya Uwanja wa Hard Rock ilipochezwa mechi hiyo zinadaiwa kusababishwa na mashabiki ambao hawakuwa na tiketi lakini walikuwa wakihaha kutaka kuingia uwanjani.
Hali hiyo ilisababisha hata wale wenye tiketi kuchelewa kuingia wakisubiri nje ya uwanja kwa muda mrefu ili kupata nafasi ya kuingia ndani.
Katika tukio hilo polisi walilazimika kupambana na mashabiki hao ambao baadhi yao walikamatwa na wengine kulazimika kupatiwa matibabu hasa ya huduma ya kwanza.
Katika hali ambayo pia haikutarajiwa muda wa mapumziko ulichelewa kwa takriban dakika 25 kwa sababu ya burudani ya muziki kutoka kwa nyota wa miondoko ya pop, Shakira ambaye pia anatokea nchini Colombia.

Kitendo cah mwanamuziki huyo kuchelewesha mechi kilionekana kumkera kocha wa Colombia, Nestor Lorenzo na baadhi ya mashabiki waliokuwa uwanjani hapo.
Kwa Messi taji hilo ni mwendelezo wa kufuta ukame wa mataji na timu yake ya taifa kwani kwa muda mrefu alikuwa hana taji la kujivunia na timu hiyo kabla ya kubeba taji lake la kwanza mwaka 2021 la Copa America wakati huo akiwa na miaka 34.
Mafanikio hayo yanamfanya awe amebeba mataji yote makubwa akiwa na timu yake ya taifa kwa miaka ya karibuni, kwani baada ya mwaka 2021, mwaka uliofuata wa 2022 alibeba Kombe la Dunia.
Messi ambaye kwa sasa ana miaka 37 kabla ya kuanza fainali hizi za Copa America alisema kwamba bado hajaamua ni lini atastaafu kuichezea timu yake ya taifa hivyo huenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 akaendelea kuiwakilisha timu hiyo.
