North Carolina, Marekani
Shirikisho la Soka nchi za Marekani Kusini (Conmebol) limeanza uchunguzi unaohusisha tukio lisilo la kiuanamichezo lililomhusisha mshambuliaji wa Uruguay, Darwin Nune ambaye alipambana na mashabiki wa Colombia.
Tukio hilo lilitokea Jumatano katika mechi ya nusu fainali ya Copa America baina ya timu hizo mbili, mechi ambayo ilimalizika kwa Colombia kutoka na ushindi wa bao 1-0.
Katika tukio hilo, Nunez ambaye pia ni mshambuliaji wa Liverpool alionekana akipambana na mashabiki jukwaani katika eneo ambalo familia za wachezaji wengi wa Colombia walikuwa wamekaa.
Nunez alionekana akiruka kutoka upande mmoja na kuelekea sehemu ya mashabiki kabla ya kuanza kupambana nao.
“Ni jambo lisilokubalika, tukio kama hili limegeuza hali ya utulivu kuwa vurugu,” ilieleza taarifa ya Conmebol.
Taarifa hiyo pia iliwahakikishia mashabiki na wadau wa soka kuwa hakuna tukio ambalo linaharibu taswira nzuri ya soka kwa kuhusisha mashabiki na wachezaji uwanjani halafu likavumiliwa.
Katika uchunguzi huo, Conmebol watataka kufahamu kiini cha tukio hilo lililotokea baada ya ushindi wa Colombia ambao Jumapili wataumana na Argentina katika mechi ya fainali.
“Hakukuwa na polisi na hivyo tulilazimika kuzilinda familia zetu, haya ni matatizo ya watu wawili au watatu ambao walipata pombe kidogo na hawajui namna ya kunywa pombe,” alisema nahodha wa Uruguay, Jose Maria Gimenez.
Nunez ambaye hajasema lolote kuhusiana na tukio hilo, mara baada ya hali ya utulivu kurejea, alionekana uwanjani akimbusu mtoto wake wa kiume.
