Cairo Misri
Timu za Tanzania zimewajua wapinzani wao katika michuano ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo Yanga wataanza na Vital’O ya Burundi, Azam FC dhidi ya APR ya Rwanda wakati Simba itaanzia raundi ya pili.
Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo iliyofanyika Alhamisi hii, Yanga na Azam zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika zikipita hatua hiyo, Yanga itacheza na mshindi kati ya Sports Club Villa ya Uganda na Commercia Bank ya Ethiopia.
Nao Azam FC kama watafanikiwa kuitoa APR baada ya ushindi huo watacheza dhidi ya mshindi wa mechi kati ya JKU ya Zanzibar dhidi Pyramids ya Misri, timu anayoichezea mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele.
Simba ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika itaanzia katika raundi ya pili kwa kucheza na mshindi wa mechi kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na timu kutoka Libya ambayo bado haijatajwa.
Kwa mtazamo wa walio wengi Yanga, Azam na hata Simba zinapewa nafasi kubwa ya kushinda mechi zao za kwanza za michuano hiyo ambayo ni ya msimu wa 2024-25 na kwenda hatua ya makundi.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Coastal Union ambao watashiriki Kombe la Shirikisho wao wataanza kwa kuikabili ya Bravos do Maguis ya Angola na kama watapita mtego wa Waangola hao mechi inayofuata wataumana na FC Lupopo ya DR Congo.
Kwa Tanzania Yanga na Simba hadi sasa ndizo timu zenye rekodi nzuri katika michuano ya klabu Afrika, Yanga ilifikia hatua ya fainali Kombe la Shirikisho mwaka 2023 wakati Simba ina rekodi nzuri ya kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa misimu minne mfululizo.
Katika msimu uliopita wa 2023-24, Yanga na Simba zote zilifikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo Yanga ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Simba ikatolewa na Al Ahly ya Misri.
Kimataifa Yanga kuanza na Vital’O CAF
Yanga kuanza na Vital’O CAF
Read also