Munich, Ujerumani
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amekiri kufeli katika mbio zake kwenye fainali za soka za Euro 2024 baada ya timu hiyo kutolewa na Hispania katika nusu fainali kwa kipigo cha mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumanne, Mbappe alitoa pasi kwa Kolo Muani na kuipatia Ufaransa bao la kwanza lakini Hispania ilijibu mapigo kwa mabao yaliyofungwa na Lamine Yamal na Dani Olmo.
Kwa ushindi huo, Hispania sasa itaumana na mshindi wa mechi kati ya England na Uholanzi katika mechi ya fainali itakayopigwa Jumapili mjini Berlin katika dimba la Olimpiki.
Mbappe ambaye anatarajia kutangazwa rasmi na klabu ya Real Madrid hivi karibuni, amemaliza fainali hizo akiwa na bao moja tu la penalti ambalo alifunga katika mechi dhidi ya Poland katika hatua ya makundi kabla ya kuumia pua.
:”Kuhusu mashindano, kwa upande wangu yalikuwa magumu, nilifeli, tulikuwa na matamanio ya kuwa mabingwa wa Ulaya, nilikuwa na matamanio ya kuwa bingwa Ulaya, haikuwa hivyo, kwa hiyo ni kufeli,” alisema Mbappe.
“Hayo ndiyo mambo ya soka, ni lazima sasa tuangalie mbele, kimekuwa kipindi kirefu cha mwaka mzima, na sasa nakwenda likizo na kupata muda wa kupumzika hilo litakuwa jambo zuri kwangu na baada ya hapo nitajitahidi nirudi nikiwa imara,” alisema Mbappe.
Mbappe amepitia kipindi kigumu katika fainali za Euro 2024 baada ya kuumia pua katika mechi ya kwanza ya Ufaransa dhidi ya Austria na kukosa mechi dhidi ya Uholanzi ingawa baadaye alicheza mechi zilizofuata akiwa amevaa kifaa maalum cha kulinda pua iliyoumia.
