Na mwandishi wetu
Wafalme wawili wa soka la Tanzania, Simba na Yanga wameendelea kutanua makucha yao baada ya leo Jumatatu kutambulisha vifaa vipya kuelekea msimu ujao wa 2024-25.
Yanga ambayo imeshawatambulisha Clatous Chama kutoka Simba na Prince Dube aliyekuwa Azam, leo pia imemtambulisha beki wa kushoto, Shadrack Boka (pichani juu) kutoka FC Lupopo.
Boka, 24 raia wa DR Congo amejiunga na miamba hiyo ya Kariakoo kurithi nafasi ya Joyce Lomalisa raia wa DR Congo pia aliyeitumika Jangwani kwa misimu miwili.
Pia Yanga imemtangaza Khomeiny Aboubakar kama kipa wao mpya kutoka Ihefu FC ambapo ataungana na makipa wengine, Djigui Diarra an Aboutwalib Mshery kupigania kulinda milingoti ya timu hiyo.
Lakini duru nyingine zimefafanua kuwa beki wao wa kulia, Kibwana Shomari ameongeza mkataba wa miaka miwili na timu hiyo, utakaomweka Yanga mpaka 2026.
Upande wa pili Simba nao wamemtangaza kiungo Yusuf Kagoma kutoka Singida Fountain Gate kuwa amejiunga na timu hiyo kwa kandarasi ya miaka mitatu.
Baada ya Kagoma, Simba sasa inakuwa imetangaza usajili wa wachezaji 12 wapya kuelekea msimu ujao.
Wakati huo huo pia kipa wa Wekundu hao, Ayoub Lakred aliyetua msimu uliopita akitokea FAR Rabat ya Morocco ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kukipiga Msimbazi.
Katika hatua nyingine, Simba imekwea pipa leo kuelekea Misri kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya michuano iliyo mbele yao msimu ujao ikiwemo michuano ya Ngao ya Jamii ambapo mechi ya kwanza wataumana na Yanga.
Yanga wao leo kikosi chao kilikuwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya mwisho kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.
Soka Yanga, Simba zaendelea kutambulisha wapya
Yanga, Simba zaendelea kutambulisha wapya
Read also
