Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga SC inatarajia kuvaana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayonolewa na Nasrredine Nabi katika mchezo maalum wa Kombe la Toyota.
Nabi atakutana na Yanga aliyoinoa msimu mmoja uliopita, Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Toyota uliopo Bloemfontein, Afrika Kusini ukiwa ni mchezo wa michuano ya kirafiki ya Kombe la Toyota.
Kaizer imeeleza uwapo wa mechi hiyo kwenye mitandao yake: “Kaizer Chiefs watakuwa wenyeji wa Yanga katika mchuano wa kwanza wa Kombe la Toyota utakaochezwa kwenye Uwanja wa Toyota mjini Bloemfontein Julai 28, 2024.”
Rais wa Yanga, Hersi Said amezungumza kuhusu mwaliko huo leo Jumatatu akisema: “Sisi kama Yanga tunafurahishwa sana na mwaliko huu wa kushiriki katika Kombe la Toyota 2024.
“Mchezo huu unaendeleza uhusiano kati ya timu zetu kubwa mbili barani Afrika ambao ulianza mwaka jana tulipowaalika Kaizer Chiefs kushiriki katika Tamasha la Wiki ya Mwananchi.
“Tunafurahia mwaliko huu na tunaahidi kutoa mchezo wa ushindani utakaotusaidia kujiandaa kwa msimu mpya wa 2024/25.”
Timu hizo mara ya mwisho zilikutana Julai 22, mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo wa Wiki ya Mwananchi ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Kennedy Musonda.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Nabi kukutana na Yanga tangu alipoondoka katika kikosi hicho msimu wa 2022-23 na kutimkia FAR Rabat ya Morocco kabla ya hivi karibuni kutua Kaizer.
Kimataifa Yanga kushiriki Kombe la Toyota
Yanga kushiriki Kombe la Toyota
Read also