Munich, Ujerumani
Klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani imemsajili kwa mkataba wa miaka mitano winga, Michael Olise kutoka klabu ya Crystal Palace ya England kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 60 milioni.
Olise, 22, mzaliwa wa England ambaye ni Mfaransa na amekuwa akiichezea timu ya Ufarnsa ya vijana chini ya miaka 21, katika misimu mitatu na Palace hadi sasa amecheza mechi 90 za mashindano yote.
Hatua ya Bayern kukamilisha usajili wa Olise linakuwa pigo kwa klabu za Chelsea na Newcastle United ambazo zote ziliweka wazi nia yao ya kutaka kumsajili mchezaji huyo ambaye hata hivyo aliamua kuichagua Bayern ambako atakuwa chini ya kocha Vincent Kompany.
“Nina furaha kubwa kwa sasa kuwa katika klabu hii kubwa, ni changamoto ya kipekee, hicho ndicho kitu pekee ninachokitaka, nataka kuthibitisha uwezo wangu katika kiwango hiki na kutoa mchango wangu kuhakikisha tunashinda mataji mengi kadri iwezekanavyo kwa miaka ijayo,” alisema Olise.
Akiwa na Palace ambayo ilimaliza nafasi ya 10 kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu England, Olise aliifungia timu hiyo mabao 10 katika ligi hiyo.
Kabla ya kuanza kuiwakilisha Bayern, Olise atakuwa na kikosi cha Ufaransa ambacho kitashiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika baadaye mwezi huu katika jiji la Paris.
“Tunajivunia kwa kiasi kikubwa kile ambacho Michael amekifanikisha akiwa Crystal Palace, klabu ambayo ameendeleza soka lake na kuwa bora, tunaheshimu uamuzi wake wa kujipima katika soka la hadhi ya juu duniani,” alisema Steve Parish, mwenyekiti wa Eagles, timu ya zamani ya Olise.
Bayern pia inadaiwa kuwa katika mkakati wa kumsajli kiungo wa Ureno, Joao Palhinha anayekipiga Fulham kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 42 milioni.
