Stuttgart, Ujerumani
Wenyeji Ujerumani wameaga fainali za Euro2 2024 baada ya kufungwa mabao 2-1 na Hispania katika mechi ya robo fainali kama ambavyo Ureno nayo imeaga fainali hizo baada ya kulala kwa penalti 5-3 mbele ya Ufaransa.
Kwa matokeo ya mechi hizo zilizopigwa Ijumaa hii jioni, Ufaransa na Hispania baada ya kushinda sasa zitakutana Jumanne katika nusu fainali ambayo mshindi wake atacheza mechi ya fainali.
Ushindi wa Hispania ulikuja baada ya mechi hiyo kupigwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare ya 1-1 na ndipo Hispania waliponeemeka kwa bao la Mikel Merino katika dakika ya 119.
Hispania walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya sita ya kipindi cha pili mfungaji akiwa Dani Olmo ambaye aliujaza wavuni mpira uliotokana na krosi ya kinda wa miaka 16, Lamine Yamal.
Ujerumani baada ya kupambana walisawazisha bao hilo dakika ya 89 mfungaji akiwa Florian Wirtz, bao lililoamsha shangwe za mashabiki wa timu hiyo mwenyeji ambao walianza kukata tamaa.
Ufaransa yaitoa Ureno
Nayo Ufaransa ilifanikiwa kuitoa Ureno kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya dakika 120 za kukata na shoka ambazo ziliisha kwa sare ya 0-0.
Ureno ambao waliitoa Slovenia katika hatua ya mtoano kwa mikwaju ya penalti walishindwa kuonesha ubora huo na kujikuta wakiziaga fainali hizo ambazo mwaka 2016 walibeba taji.

Macho ya mashabiki walio wengi yalikuwa kwa nyota wa Ureno mwenye miaka 39, Cristiano Ronaldo ambaye alisema kwamba fainali za Euro 2024 ni za mwisho kwake hivyo hatokuwapo kwenye fainali za 2028.
Ronaldo hata hivyo hakuweka wazi hatma yake kwenye timu ya taifa kwa ujumla kama ataendelea kuichezea kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 au la.
Mbali na Ronaldo, mchezaji mwingine ambaye aliteka hisia za mashabiki kabla ya mechi hiyo ni Kylian Mbappe wa Ufaransa lakini si yeye wala Ronaldo aliyeweza kuwa msaada kwa timu yake.
Kwa Mbappe ambaye anavaa kifaa maalum cha kuzuia pua iliyovunjika katika mechi ya kwanza dhidi ya Austria, hali ilikuwa mbaya zaidi kwani alitolewa na hivyo kutokuwamo katika mikwaju ya penalti.
