Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imemtangaza, Fadlu Davids kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo akichukua nafasi ya Juma Mgunda aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo.
Taarifa iliyopatikana kwenye mitandao ya klabu hiyo Ijumaa hii ilimtaja kocha huyo pamoja na jopo la wasaidizi wake katika benchi la ufundi.
Wasaidizi waliotajwa ni kocha msaidizi, Darian Wilkens, kocha wa makipa, Wayne Sandilands, kocha wa viungo Riedoh Berdien na mchambuzi wa mechi Muez Kaje ambao kama alivyo Davids wote wanatokea Afrika Kusini.
Kabla ya kumalizika Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-24, Simba iliondokewa na kocha wake Abdelhak Benchikha na Mgunda kukaimu nafasi hiyo katika mechi chache zilizobaki kabla ya msimu kumalizika.
Simba ilimaliza ligi hiyo ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam FC na sasa itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika katika msimu ujao wa 2024-25.
Taarifa za vyanzo mbalimbali vya habari zinaonesha kuwa Davids aliwahi kuwa mshambuliaji wa timu kadhaa nchini Afrika Kusini kabla ya kustaafu soka mwaka 2012 na kujikita katika kazi ya kocha.
Amewahi kuzinoa timu kadhaa lakini zilizomjengea heshima ni Maritzburg United ambayo amewahi kuwa kocha msaidizi na baadaye kocha wa muda na alionesha uwezo wake zaidi katika msimu wa 2018-19.
Na ingawa baadaye alitimuliwa lakini alisifiwa kwa kuibadili timu ambayo ilikuwa katika mwelekeo mbaya na kuifanya iwe ya ushindani hadi kukosa pointi chache za kufuzu michuano ya CAF.
Timu nyingine ambayo Davids alionesha uwezo ni Orlando Pirates, alijiunga nayo mwaka 2019, sifa kubwa ya kocha huyo katika timu hiyo pia ni uwezo wake wa kuibadili kiuchezaji na kuwaendelea wachezaji vijana.
Soka Davids kocha mpya Simba
Davids kocha mpya Simba
Read also