Manchester, England
Klabu ya Manchester United imemuongezea mkataba kocha Erik ten Hag ambao sasa utamfanya aendelee kuwa na klabu hiyo hadi mwaka 2026 ikiwa ni mwaka mmoja zaidi ya mkataba wa sasa unaoishia 2025.
Sambamba na hilo, klabu hiyo inaendelea kufanya maboresho ya maofisa wake wakiwamo wa benchi la ufundi huku kukiwa na habari kuwa Ruud van Nistelrooy na Rene Heke wapo mbioni kujiunga na klabu hiyo.
Ten Hag alisema kwamba ana furaha kwa kufikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo kwa lengo la kuendelea kufanya kazi pamoja.
“Tukiangalia miaka miwili iliyopita tunaweza kutafakari tukiwa wenye kujivunia mataji mawili na mifano mingi ya hatua za mafanikio kutoka pale ambapo tulikuwa wakati najiunga na klabu hii,” alisema Ten Hag.
Ten Hag hata hivyo aliweka wazi kuwa pamoja na mafanikio hayo ni lazima wawe wazi kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufikia kiwango kinachotarajiwa katika klabu hiyo ambacho ni kupigania mataji ya England na Ulaya.
Alisema kwamba katika mazungumzo yake na uongozi wa klabu hiyo wamekuwa wamoja katika dira yao ya kuhakikisha wanafikia malengo hayo na wako pamoja na imara katika kuhakikisha safari hiyo inakuwa ya pamoja.
Ten Hag alijiunga na Man United mwaka 2022 akitokea Ajax ya Uholanzi na kusaini mkataba ambao ulitarajiwa kufikia ukomo mwaka 2025 kabla ya kuongezwa hii leo Alhamisi na sasa utafikia ukomo ifikapo Juni 2026.