Johannesburg, Afrika Kusini
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepangwa Kundi H katika kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, kundi ambalo pia lina timu za Ethiopia, DR Congo na Guinea.
Katika droo iliyofanyika leo jijini Johannesburg, mabingwa watetezi, Ivory Coast wao wamepangwa Kundi G ambalo pia lina timu za Sierra Leone, Zambia pamoja na Chad.
Jumla ya timu 48 zitachuana katika mbio za kuwania kufuzu fainali hizo zinazoshirikisha nchi za mataifa ya Afrika ambapo timu hizo zimepangwa katika makundi 12, kila kundi likiwa na timu nne ambapo mbili ndizo zitakazofuzu.
Morocco ambao wapo Kundi B wanakuwa wamefuzu moja kwa moja kama wenyeji na hiyo maana yake ni kwamba timu nyingine mbili katika kundi lake kati ya Gabon, Afrika ya Kati na Lesotho ndizo zitakazofuzu.
Mechi za kuwania kufuzu fainali hizo zitaanza kutimua vumbi Septemba na kuendelea Oktoba hadi Novemba na fainali za Afcon 2025 zitaanza kutimua vumbi Desemba 21 hadi Januari 18 2026 siku ambayo mechi ya mwisho itapigwa na bingwa kupatikana.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa fainali za Afcon kuchezwa Desemba na kuendelea hadi wakati wa Krismasi kipindi ambacho baadhi ya ligi Ulaya zinakuwa na mapumziko mafupi.