California, Marekani
Brazil imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya soka ya Copa America inayoendelea Marekani baada ya sare ya bao 1-1 na Colombia jana Jumanne ingawa matokeo hayo yameibua hofu kuhusu ubora wa timu hiyo.
Kwa matokeo hayo Colombia imeshika usukani Kundi D na sasa inasubiri kuumana na Panama katika robo fainali wakati Brazil iliyoshika nafasi ya pili itaumana na Uruguay ambao ni vinara wa Kundi C.
Brazil ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Raphinha katika dakika ya 12 kwa mpira wa adhabu lakini dakika chache kabla ya timu kwenda mapumziko Colombia walisawazisha bao hilo mfungaji akiwa ni Daniel Munoz.
“Ni mechi ambayo sote tulitaka kuicheza ili kuipima timu kwenye tukio kubwa, nafikiri tumepiga hatua mbele,” alisema kocha wa Colombia Nestor Lorenzo.
Lorenzo alisema kwamba unapocheza na Brazil huwezi kupuuza hata sekunde moja, na hivyo kwa mtazamo wao wameridhika na sasa wanaifikiria mechi yao dhidi ya Panama.
Brazil pia ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake, VinÃcius Júnior kupewa kadi ya njano dakika ya saba na hivyo ataikosa mechi dhidi ya Uruguay kutokana na kuwa na kadi nyingine hapo kabla.
Matokeo hayo kwa ujumla yameshangaza wengi akiwamo beki wa Brazil Marquinhos ambaye amekiri kwamba wanahitaji kuwa katika ubora.
“Ni lazima tuwe wakweli sisi wenyewe kwamba tuna kazi ya kufanya ili tuwe bora zaidi hasa katika mashindano makubwa kama haya,” alisema Marquinhos .
