Na mwandishi wetu
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) kimeandaa mbio za marathon zenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kumtua mama kuni kichwani.
Taarifa ya Taswa iliyotolewa leo Jumanne na kusainiwa na kaimu katibu mkuu wa chama hicho, Imani Makongoro ilieleza kuwa mbio hizo zilizopewa jina la Mwambao Marathon zitafanyika jijini Tanga Septemba 29 mwaka huu.
Mbio hizo zimeandaliwa na Taswa ili kusukuma mbele dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka hadi 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Taswa chini ya mwenyekiti wake, Amir Mhando (pichani) pia inakaribisha mashirika, makampuni, wadau wa mazingira na nishati safi kushirikiana nao katika kuandaa mbio hizo ambazo washiriki watashiriki mbio za kilometa 21, 10 au za kujifurahisha za kilometa tano.
Sambamba na hilo, mkutano mkuu wa wanachama wa Taswa utafanyika Septemba 28 mwaka huu jijini Tanga na kuhusisha wanachama waliolipa ada na mwisho wa kulipa ada na kuthibitisha kushiriki ni Agosti 30 mwaka huu.
Wanachama washiriki wa mkutano huo pia watapata nafasi ya kuhudhuria semina kuhusu umuhimu wa waandishi wa habari za michezo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Katika semina hiyo pia itatolewa mada maalum kuhusu nafasi ya wanahabari kuelekea fainali za soka za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 au Afcon 2027 ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji pamoja na nchi za Kenya na Uganda.
Sports Mix Taswa yaandaa Mwambao Marathon
Taswa yaandaa Mwambao Marathon
Read also
