Munich, Ujerumani
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps ana matumaini nahodha na mshambuliaji wa timu hiyo, Kylian Mbappe atakuwa uwanjani leo Jumanne katika mechi ya fainali za Euro 2024 dhidi ya Poland.
Mbappe aliumia pua katika mechi ya kwanza ya Ufaransa dhidi ya Austria na kulikuwa na matarajio makubwa kwamba angecheza Ijumaa iliyopita katika mechi dhidi ya Uholanzi lakini aliishia kusugua benchi.
Mchezaji huyo hata hivyo ameweza kufanya mazoezi ya hapa na pale ya timu hiyo na kuonekana yuko vizuri ambapo katika mkutano na waandishi wa habari, Deschamps alisema kwamba Mbappe yuko tayari kurejea uwanjani.
“Anakuwa vizuri kila baada ya siku, alikuwa katika mazoezi yetu, michubuko imeanza kuwa tofauti na awali, ameanza kuzoea kifaa anachovalishwa usoni,” alisema Deschamps.
Deschamps alisema kwamba Mbappe anataka kucheza na amekuwa mwenye shauku kubwa ya kucheza, awali alitaka acheze mechi dhidi ya Uholanzi lakini kwa sasa anataka kucheza mechi ya kesho (leo).
“Niwe tu mkweli tukiwa mazoezini nilisahau hata kama kuna kitu anavaa usoni, alikuwa vizuri, tishio, alicheza vizuri hasa kwenye mazoezi, natarajia itakuwa hivyo hivyo kwenye mechi hapo kesho (leo) alisema Deschamps.
