London, England
Washambuliaji wa zamani wa England, Gary Lineker na Alan Shearer wameshikilia msimamo wao wa kumshutumu mshambuliaji wa sasa wa timu hiyo, Harry Kane kutokana na kiwango cha timu hiyo katika mechi na Denmark.
England na Denmark zilitoka sare ya bao 1-1 katika fainali za Euro 2024 zinazoendelea Ujerumani, matokeo yaliyoifanya England ifikishe pointi nne huku Kane akishutumiwa na washambuliaji hao wa zamani kwa kucheza chini ya kiwango.
Kane hata hivyo baada ya shutuma hizo aliwataka Lineker na Alan Shearer ambao kwa sasa ni wachambuzi kuitambua thamani ya jezi ya England kabla ya kuishutumu timu hiyo inayonolewa na kocha Gareth Southgate.
Katika tathmini yao kuhusu mechi ya England na Denmark, Shearer na Lineker hawakufurahishwa na kiwango cha timu huku wakimshutumu Kane ambaye baadaye aliwajibu lakini wote wameibuka tena kushikilia msimamo wao.
Shearer alimtaka Kane ajibu hoja zao uwanjani na si vinginevyo na kusisitiza uwanjani ndiko majibu sahihi yanapoweza kupatikana wakati Lineker alisema waandishi ni kama wanalishabikia jambo hilo.
“Tumekuwa tukilalamikia kiwango cha England kama ilivyo kwa waandishi wengine lakini mnajua kilichotokea, pia tumewahi kuzungumzia mara kadhaa kuhusu waandishi kukosa busara za kutosha kuuliza maswali yao,” alisema Lineker.
“Jambo la muhimu ni kwamba hili halijawa suala binafsi, hicho ndicho kitu muhimu, walikuwa hovyo na ni lazima tuseme kama England wangekuwa vizuri pia tungesema wako vizuri, hivyo ndivyo mambo yalivyo,” alisema Shearer.
“Ukiwa mchezaji wakati wote unatakiwa kuwa na namna nzuri ya kutoa majibu uwanjani, sina tatizo na alichokisema lakini siwezi kubadili hata kimoja katika niliyoyasema,” aliongeza Shearer.
England leo Jumanne jioni itacheza mechi yake ya mwisho ya Kundi C dhidi ya Slovenia, mechi itakayopigwa mjini Cologne.
Mechi za leo Jumanne Euro 2024
Kundi C
England vs Slovenia
Denmark vs Serbia
Kundi D
Uholanzi vs Austria
Ufaransa vs Poland
Kimataifa Lineker, Shearer wamkomalia Kane
Lineker, Shearer wamkomalia Kane
Read also
