Munich, Ujerumani
Arda Guler au Messi wa Uturuki ndio kwanza ana miaka 19, kesho Jumamosi ataiwakilisha timu hiyo dhidi ya Ureno yenye Cristiano Ronaldo, 39, huku Arda akiwa tayari ameweka rekodi ya kuvutia kwenye fainali za Euro 2024.
Rekodi ya Arda imekuja baada ya kufunga bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Georgia na hapo hapo kuibuka nyota wa mchezo huo na sasa anasubiriwa kwa mara nyingine kuonesha uwezo huo katika mechi na Ureno.
Katika mechi na Georgia iliyopigwa Jumanne iliyopita imemfanya Arda aweke rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa umri mdogo (miaka 19 na siku 114) kufunga goli katika mechi yake ya kwanza ya fainali za Euro.
Arda sasa anaingia katika rekodi ya wachezaji wa umri mdogo kufunga goli kwenye mechi zao za kwanza za fainali hizo zinazoshirikisha nchi wanachama wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa).

Katika orodha hiyo pamoja na Arda wengine ni Ferenc Bene wa Hungary aliyefunga bao dhidi ya Hispania kwenye fainali za mwaka 1964 na Cristiano Ronaldo wa Ureno ambaye alifunga dhidi ya Ugiriki mwaka 2004.
Ukiweka kando rekodi hizo na uwezo ambao tayari ameuonesha, kesho Jumamosi atalazimika kuonesha tena uwezo huo wakati Uturuki ikiumana na Ureno ya Cristiano Ronaldo.
Mashabiki Uturuki wamekuwa na matarajio makubwa na Arda ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Real Madrid ya Hispania ambayo alijiunga nayo Julai mwaka jana akitokea Fenerbahce ya Uturuki.
“Nina furaha, sina namna ya kuelezea ninavyojisikia, nimekuwa nikiota kufunga bao la aina hii, ninafanya juhudi zaidi ili kurudisha fadhila kwa mapenzi ya kipekee ninayoyapata,” alisema Arda.
“Nimekuwa nikifanyia mazoezi upigaji wa mashuti ya aina hii kila baada ya mazoezi, na sasa nina furaha kubwa kufunga katika namna hii, kocha (wa Real Madrid) Carlo Ancelotti alinitumia ujumbe akinitakia heri,” alisema Arda.
Akiwa Real Madrid amefunga mabao matano msimu mzima wakati timu hiyo imebeba taji la La Liga na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo pia limemfanya Arda awe mchezaji wa kwanza kutoka Uturuki kubeba taji la ligi hiyo.
Uturuki hata hivyo wana kazi ngumu dhidi ya Ureno, ni mechi ambayo pia inaweza kuwa nafasi nyingine kwa Arda kudhihirisha ubora wake uliomfanya afananishwe na Lionel Messi, ubora uliowashawishi Real Madrid wamsajili.
Katika mechi hiyo, Ronaldo mwenye miaka 39 na mmoja wa wachezaji gumzo kwenye fainali za Euro 2024, anatarajia kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Uturuki yenye Arda ambaye Ronaldo amemzidi umri kwa miaka 20.
