Frankfurt, Ujerumani
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate ameeleza kutofurahishwa na kiwango cha timu yake kwenye fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea Ujerumani licha ya kushinda mechi moja na kutoa sare moja.
Jana Alhamisi, England ilitoa sare ya bao 1-1 na Denmark, matokeo ambayo yamewafanya washike usukani katika Kundi C na kujiweka pazuri kufuzu hatua ya mtoano inayoshirikisha timu 16.
England ambayo ilianza fainali hizo kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 mbele ya Serbia hata hivyo, imeshindwa kuutawala vyema mchezo dhidi ya Denmark na haikuwa katika kiwango bora.
Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Frankfurt, England ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 18 lililofungwa na Harry Kane na Denmark walisawazisha kupitia Morten Hjulmand dakika ya 34.
“Tunaelewa kuwa watu watakuwa wamesikitishwa na kiwango na hivyo ni lazima tucheze vizuri na kuwa bora zaidi,” alisema Southgate.
Juhudi za England kusaka bao la kuongoza hazikuweza kuzaa matunda, kama wangepata bao hilo lingeweza kuwafanya wafuzu hatua inayofuata moja kwa moja wakiwa na mechi moja mkononi.
“Kwa wakati huu hatujautumia vizuri mpira kiasi cha kutosha na ni lazima tukubali kwamba kama hufanyi hivyo utaweza kukwama kama ambavyo imekuwa kwetu, tunajua kwamba kuna kiwango ambacho tunalazimika kukitafuta,” alisema Southgate.
England itakamilisha mechi yake ya hatua ya makundi dhidi ya Slovenia, katika mechi itakayopigwa Jumanne ijayo mjini Cologne.
