Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeweka wazi leo Jumanne kuachana na kiungo mshambuliaji wake, Saido Ntobazonkiza baada ya kudumu Msimbazi kwa msimu mmoja na nusu.
Taarifa hiyo imetolewa na Simba kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii ambapo imetoa shukrani kwa mchezaji huyo raia wa Burundi kwa utumishi wake katika muda wote aliokuwepo hapo.
Saido aliyewahi kukipiga Yanga msimu wa 2020-21 ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo katika msimu wa 2023-24 uliomalizika hivi karibuni ambapo alitupia mabao 11.
Katika msimu wake wa kwanza kutua Simba katika dirisha dogo la 2022-23 alifunga mabao 17 na kufungana ufungaji bora wa Ligi Kuu NBC na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele anayekipiga Pyramid ya Misri kwa sasa.
Saido mmoja wa wachezaji mahiri na mwenye uhakika kwenye mikwaju ya penalti pia aliwahi kung’ara na timu ya Geita Gold mara baada ya kuondoka Yanga.
Hatua ya Simba kuachana na mchezaji huyo inawafanya wachezaji walioachwa kuwa wawili baada ya aliyekuwa nahodha, John Bocco ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Simba chini ya miaka 17 naye kupewa mkono wa kwaheri.
Soka Saido aachwa Simba
Saido aachwa Simba
Read also