Munich, Ujerumani
Nahodha na beki wa timu ya taifa ya Uholanzi, Virgil van Dijk amesema kwamba timu yao ni lazima imzuie Kylian Mbappé kwa pamoja badala ya kutegemea mtu mmoja aifanye kazi hiyo.
Ufaransa na Uholanzi zinakutana Juni 21 katika mechi ya Kundi D kwenye fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani mechi zote zikiwa katika hatua ya makundi.
Uholanzi tayari imeshaandika ushindi wake wa kwanza katika fainali hizo baada ya kuinyuka Poland mabao 2-1 na sasa itahitaji kushinda mechi ya pili dhidi ya Ufaransa ili kujiweka mguu sawa kwa ajili ya kucheza hatua ya mtoano.
Namna mojawapo ya vijana hao wanaonolewa na Ronaldo Koeman kushinda mechi na Ufaransa kwa mujibu wa Van Dijk ni kuhakikisha wanamdhibiti Mbappe, nyota wa PSG ambaye inadaiwa amekamilisha mipango ya kujiunga na Real Madrid.
“Angalia, kila mmoja anajua ubora wake, lazima tuwe katika ubora wetu kama timu ili kumzuia (Mbappe) asifunge lakini vyovyote ilivyo yeye ni mchezaji wa hadhi ya juu duniani, katika sekunde chache tu anaweza kubadili mambo” alisema Van Dijk.
Van Dijk ambaye pia ni beki wa Liverpool anasema ni lazima wawe tayari kama timu kwa mtihani wa aina hiyo na anadhani tayari Uholanzi wameonesha wanachokiweza katika mechi kadhaa zilizopita.
“Tuna safu ya ulinzi iliyo tayari kwa ajili ya majaribu hayo hapo Ijumaa, hiyo kwa sasa ni mechi kubwa, tuliwapa tabu kidogo katika mechi chache zilizopita dhidi yao, lakini kwa sasa najiandaa kwa mechi hiyo, ni suala la kuwa tayari kwa mtihani mkubwa wa aina hiyo,” alisema Van Dijk.