London, England
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate amesema kwamba fainali za Kombe la Ulaya au Euro 2024 huenda ikawa nafasi ya mwisho kwake kubeba taji akiwa kocha wa timu hiyo.
Kauli ya kocha huyo imekuja huku ikifahamika kuwa mkataba wake na timu ya England unafikia ukomo Desemba mwaka huu na hivyo kutoa kila dalili kwamba haya huenda ni mashindano yake ya mwisho makubwa akiwa kocha England.
Habari nyingine hata hivyo zinadai kuwa Chama cha Soka England (FA) kinadaiwa kujipanga ili kumshawishi aendelee kuinoa timu hiyo hadi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo zitafanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Pamoja na kuwapo mpango huo lakini Southgate amenukuliwa na chanzo kimoja cha habari akisema kwamba iwapo England itashindwa kubeba taji hilo nchini Ujerumani huo huenda ukawa ndio mwisho wake na timu hiyo.
“Kama hatutashinda huenda nisiwe hapa tena, hivyo hii inaweza kuwa nafasi yangu ya mwisho, kama nataka kuwa timu kubwa na nataka kuwa kocha wa hadhi ya juu hapo ni lazima kufanya makubwa katika mashindano makubwa,” alisema Southgate.
Southgate, 53 amekuwa kocha wa England tangu mwaka 2016 na anajivunia rekodi ya kuiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018, fainali Euro 2020 na robo fainali Kombe la Dunia 2022.
