Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Jr amesema kwamba amegeuka kuwa mhanga wa ubaguzi wa rangi baada ya mashabiki watatu waliomfanyia dhihaka za kibaguzi kufungwa jela miezi minane.
Mashabiki hao wanaotajwa kuwa ni wa klabu ya Valencia walipewa adhabu hiyo baada ya kubainika kumfanyia dhihaka hizo Vinicius Mei mwaka jana katika mechi ya La Liga kati ya Real Madrid na Valencia iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mestalla.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama moja ya Valencia, mashabiki hao wamekutwa na hatia ya kufanya jinai inayohusu ukosefu wa maadili unaosababisha kuwapo ubaguzi wenye dhamira ya kubagua rangi ya mtu.
“Mimi si mlengwa wa ubaguzi, mimi ni mhanga wa ubaguzi, mhusika wa jinai ya kwanza kukutwa na hatia katika historia ya Hispania haikunihusu mimi, ni watu wote weusi,” alisema Vinicius ambaye aliwahi kumwaga chozi mbele ya wanahabari akizungumzia ubaguzi wa rangi.
Hii ni mara ya kwanza mtuhumiwa wa ubaguzi wa rangi katika soka Hispania kuadhibiwa chanzo kikiwa ni malalamiko yaliyowasilishwa moja kwa moja na mamlaka ya La Liga.
Adhabu ya kifungo cha miezi 12 ya awali ilipunguzwa baada ya makubaliano yaliyofikiwa wakati wa hatua za awali za uchunguzi wa kadhia hiyo.
Mashabiki hao pia wamepigwa marufuku kuingia katika uwanja wowote wa soka kwa miaka miwili kwenye mechi za La Liga au mechi zozote zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Hispania.
Akizungumzia hukumu hiyo rais wa La Liga, Javier Tebas alisema ni habari kubwa katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Hispania.
Alisema hukumu hiyo pia inatuma ujumbe kwa wanaoumizwa na kadhia hiyo na wale wote ambao wanakwenda kwenye viwanja vya soka ili kufanya matukio ya kibaguzi ambao La Liga wataendelea kuwataja na kuwashitaki kwa makosa ya kijinai.
