Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeelezwa kupata hasara ya Sh bilioni 1 ingawa hasara hiyo imeonekana si lolote ikifunikwa na mafanikio ambayo timu hiyo imeyapata katika msimu huu wa 2023-24 uliomalizika hivi karibuni.
Hasara hiyo imebainishwa katika mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Jumapili baada ya ripoti ya mapato na matumizi kuwasilishwa mbele ya wanachama na mkurugenzi wa fedha wa klabu hiyo, Sabri Sadick.
Katika mchanganuo uliowasilishwa kwenye mkutano huo, Yanga chini ya Injinia Hersi Said inadaiwa kukusanya mapato yaliyofikia Sh bilioni 21.1 lakini matumizi yalifikia zaidi ya Sh bilioni 22.
Hasara ya Sh bilioni moja inaweza kuonekana kuwa ni kubwa katika mazingira ya kawaida lakini mafanikio ambayo klabu hiyo imeyapata yametosha kuwafariji wanachama kiasi cha kushindwa kuhoji hasara hiyo.
Miongoni mwa mafanikio ambayo Yanga imeyapata msimu huu ni pamoja na kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kubeba taji la Ligi Kuu NBC na lile la Shirikisho CRDB.
Yanga pia msimu huu imewafanya mashabiki wake kutembea vifua mbele wakijivunia kandanda safi na kuwa na mfungaji mwenye kuongoza kwa mabao mengi katika ligi hiyo, Stephane Aziz Ki.
Timu hiyo imefanikiwa kusajili wachezaji wa hadhi ya juu barani Afrika ambao licha ya kutamba nchini pia waliweza kuzitetemesha timu kadhaa barani Afrika katika ligi ya mabingwa ikiwamo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga na Mamelodi zilikutana katika hatua ya robo fainali ya ligi hiyo kubwa barani Afrika na ingawa ni Mamelodi waliosonga mbele kwa mikwaju ya penalti lakini Yanga ilionesha uwezo wa hali ya juu.
Katika mechi hiyo Yanga ilifanikiwa kupata bao ambalo lilifungwa na Aziz Ki, bao ambalo mbele ya wengi akiwamo rais wa CAF, Patrick Motsepe lilionekana kuwa halali lakini mwamuzi alilikataa.
Sambamba na hilo Yanga pia msimu huu imewaweka katika wakati mgumu mahasimu wao Simba kwa kuwafunga katika mechi zote mbili za ligi kuanzia kipigo cha mabao 5-1 na kile cha 2-1 katika mechi ya marudiano ya ligi hiyo.
Soka Mafanikio yafunika hasara ya bilioni 1 Yanga
Mafanikio yafunika hasara ya bilioni 1 Yanga
Read also
