Manchester, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford amekiri mahakamani kosa la kuendesha gari kwa mwendo wa kasi katika barabara ambayo mwendo huo hauruhusiwi.
Rashford alikamatwa Desemba mwaka jana katika jiji la Manchester akiwa anaendesha gari lake la bei mbaya aina ya Rolls-Royce kwa kasi iliyozidi mwendo wa kawaida ambao unaruhusiwa katika eneo hilo.
Mchezaji huyo hata hivyo hakuwapo katika mahakama hiyo ya jijini Manchester wakati shauri hilo likisomwa na huenda akakutana na adhabu kali ya faini au marufuku ya kuendesha gari.
Rashford amekuwa na msimu mbaya na klabu yake akiifungia mabao manane tu na hayumo kwenye kikosi cha England kinachojiandaa kwa fainali za Euro 2024 zitakazofanyika nchini Ujerumani hivi karibuni.
Sambamba na kesi hiyo, Septemba mwaka jana, Rashford pia aliingia matatani baada ya gari lake kugongana na gari jingine wakati akitoka kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Carrington.
Ajali hiyo hata hivyo haikuwa kubwa kwani hakuna mtu yeyote aliyeumia au kupelekwa hospitali japo kwa uchunguzi na hakuna aliyekamatwa au kuhojiwa na polisi.
Mwezi uliopita Rashford alitangaza kujiweka kando na mitandao ya kijamii ili apate wasaa wa kupumzika na kujiweka sawa kifikra baada ya kupitia katika msimu mgumu wa 2023-24.
Kimataifa Rashford matatani kwa kuendesha gari kwa kasi
Rashford matatani kwa kuendesha gari kwa kasi
Read also
