Na mwandishi wetu
Wakati Azam FC ikiendelea kutangaza vifaa vipya kwa kuweka wazi usajili wa mshambuliaji Adam Adam, beki wao Edward Manyama naye ametangaza kuihama timu hiyo.
Manyama ameweka wazi taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akiwaaga mashabiki wa Azam na wachezaji wenzake akiwatakia kila heri.
“Kwa heri Azam FC, kwa heri Chamazi, ni ngumu sana ila ni wakati sahihi wa mimi kuondoka kwenye familia ya Azam, nimeshindwa hata kuandika sababu ya upendo wenu wafanyakazi, wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, mashabiki, nawatakia maisha yenye furaha na malengo tele. Mungu awabariki sana sana,” aliandika Manyama.
Upande wa Adam ambaye ni kama amerejea nyumbani baada ya kuitumikia timu hiyo kwenye kikosi cha vijana takriban miaka 10 iliyopita, imeelezwa kutua kwake ni chaguo la benchi la ufundi.
Benchi la ufundi la Azam inadaiwa limeridhishwa na kiwango alichoonesha msimu uliopita akiwa na Mashujaa na kufunga mabao saba.
Adam aliyewahi kukipiga JKT Ruvu, Polisi Dodoma, Mtibwa Sugar, Ihefu, Lipuli na timu nyinginezo ametua Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja, unaotarajiwa kuongezwa kulingana na kiwango atakachoonesha.
Wachezaji wengine waliosajiliwa Azam hadi sasa kuelekea msimu ujao ni kiungo mshambuliaji wa Ivory Coast, Franck Tiesse, kiungo Mcolombia, Ever Meza, mshambuliaji wa Colombia, Jhonier Blanco huku wakimuongezea mkataba wa miaka miwili beki wao wa kulia, Nathan Chilambo.
Soka Manyama aaga Azam, Adam asajiliwa
Manyama aaga Azam, Adam asajiliwa
Read also