Yaounde, Cameroon
Soka la Cameroon limeingia katika sintofahamu baada ya kikao kati ya kocha mkuu wa timu ya taifa, Marc Brys na Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (Fecafoot), Samuel Eto’o kuingia katika mzozo uliotawaliwa na hasira.
Brys, aliteuliwa na waziri wa michezo Cameroon, Narcisse Kombito kuwa kocha mkuu wa timu hiyo mapema mwezi uliopita na kikao chake na Eto’o kilichofanyika jana Jumanne kilikuwa cha kwanza baada ya uteuzi huo.
Eto’o alimualika Brys kwa ajili ya kilichoitwa ‘kikao kazi’ wakati Cameroon ikijiandaa kwa mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwezi ujao lakini baadhi ya wasaidizi wa Brys ambao pia waliteuliwa na waziri walizuiwa kuingia katika jengo la ofisi za Fecafoot mjini Yaounde.
Baadhi ya picha zilizopatikana kwenye mitandao ya kijamii zilimuonesha Eto’o akimkaribisha Brys katika ofisi za Fecafoot lakini muda mfupi baadaye hali ilibadilika na kutawaliwa na utata.
Eto’o baadaye akionekana mwenye hasira aliwafukuza maofisa kutoka wizara ya michezo ambao walitaka kushiriki kikao hicho na baadaye kuanza kutoleana lugha kali na Brys ambaye muda mfupi baadaye aliamua kuondoka.
Fecafoot wanatarajia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo ambalo limekuja licha ya wao kuonesha utayari wa kufanya kazi na Brys, kocha kutoka Ubelgiji ambaye awali hawakuunga mkono uteuzi wake.

Kwa kawaida uteuzi wa kocha mkuu wa timu ya taifa hufanywa na mashirikisho ya soka ingawa kwa Cameroon na baadhi ya nchi Afrika kazi hiyo hufanywa na serikali hasa mashirikisho hayo yanapokuwa na matatizo kifedha.
Serikali ya Cameroon imekuwa na kawaida ya kuingilia mambo ya soka hasa rais mkongwe wa nchi hiyo, Paul Biya ambaye inadaiwa amekuwa akihusika hadi kwenye uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa.
Inadaiwa Rais Biya ndiye aliyeshinikiza mshambuliaji mkongwe Roger Milla awemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo iliyoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990.
Milla aliitwa katika kikosi hicho akiwa na miaka 38 ambapo alifunga mabao muhimu na kuiwezesha Cameroon kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Kwa sasa timu ya taifa ya Cameroon au Indomitable Lions, inajiandaa kucheza mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Cape Verde, mechi itakayopigwa Juni 8 na siku tatu baadaye itacheza na Angola.
Cameroon imepangwa Kundi D na katika mechi mbili za kwanza ikiwa nyumbani iliifunga Mauritius na kutoka sare ugenini dhidi ya Libya wakati huo timu ikinolewa na Rigobert Song ambaye Fecafoot haikumuongezea mkataba mwingine.
