Na mwandishi wetu
Meneja habari na mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema anaamini kutokuwepo kwao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kuna kitu kitapungua kwenye michuano hiyo msimu ujao.
Ally ameyasema hayo leo Jumatano akieleza kwa kifupi kuwa hiyo inatokana na ukubwa wao kwa sasa, ubora, hamasa ya mashabiki na heshima waliyonayo ingawa hayo hawayatazami sana zaidi ya kujipanga kwa ajili ya ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Simba imeshindwa kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza Ligi Kuu NBC nafasi ya tatu kwa pointi 69 sawa na Azam iliyomaliza ya pili lakini yenyewe ikiwa juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.
“Nimelipokea kwa moyo mkunjufu Kombe la Shirikisho sababu ni michuano halali na rasmi ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) japo hatukupenda kushiriki Shirikisho, malengo yetu ni Ligi ya Mabingwa lakini imekuwa bahati mbaya tumeangukia Shirikisho hatuna budi kushiriki…
“Ingawa Simba tuna heshima yetu kwenye michuano ya Caf hasa Ligi ya Mabingwa kutokana na ukubwa wetu, ‘vibe’ letu, ubora wetu na heshima yetu. Kukosekana Ligi ya Mabingwa kuna kitu kinapungua kwenye michuano hiyo lakini huo si muda wake kwa sasa, kilichopo sasa ni kuona namna gani tunakwenda kutawala Kombe la Shirikisho msimu ujao,” alieleza Ally.
Mara ya mwisho Wekundu hao kushiriki Kombe la Shirikisho ilikuwa msimu wa 2022-23 kabla ya kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye hatua ya robo fainali kwa penalti 4-3 baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani kwake.
Timu nyingine iliyoungana na Simba kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano hiyo ni Coastal Union iliyomaliza nafasi ya nne wakati vinara Yanga na Azam zitawakilisha nchi katika ya Ligi ya Mabingwa.
