Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Stephanie Aziz Ki ameibuka kinara wa mabao Ligi Kuu NBC akimfunika kiungo wa Azam FC, Feisal Salum wakati ndoto za Simba kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo zikiota mbawa.
Aziz Ki na Feisal au Fei Toto wamekuwa katika mpambano wa kusaka kiatu cha mfungaji bora na kabla ya mechi za leo Jumanne za kufunga pazia la ligi hiyo, kila mmoja alikuwa na mabao 18.
Mabao ya mechi za leo ndiyo yaliyombeba Aziz Ki na kumfanya amalize ligi hiyo akiwa na mabao 21 baada ya Yanga kuinyuka Prisons mabao 4-1 wakati Fei amefikisha mabao 19 baada ya kufunga bao moja dhidi ya Geita Gold.
Aziz Ki leo amefunga mabao matatu peke yake na hivyo kuondoka na mpira hali ambayo si tu imedhihirisha uwezo wake katika kuzifumania nyavu bali pia amewanyamazisha waliokuwa na fikra kwamba Fei leo angeweza kumpiku kwa mabao.
Fei ambaye amewahi kucheza pamoja na Aziz Ki katika kikosi cha Yanga hata hivyo naye ana kila sababu ya kujivunia mabao aliyofunga msimu huu kwani ndiyo yaliyoiwezesha Azam kushika nafasi ya pili.
Kwa kushika nafasi ya pili, Azam itaungana na Yanga katika ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba iliyoangukia nafasi ya tatu itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na Coastal Union.
Yanga iliyotwaa taji hilo imemaliza ligi na pointi 80, Simba na Azam zimemaliza kila moja ikiwa na pointi 69, Simba imezipata pointi hizo baada ya kuifunga JKT Tanzania mabao 2-0 na Azam imeilaza Geita Gold mabao 2-0.
Azam imeshika nafasi ya pili kutokana na wastani mzuri wa mabao, imefunga mabao 63 dhidi ya 53 ya Simba wakati Azam pia imefungwa mabao 21, Simba imefungwa mabao 29.
Wakati hali ikiwa hivyo katika nafasi nne za juu, mambo si mazuri kwa Mtibwa Sugar ambayo tayari imeshuka daraja ikiungana na Geita Gold katika mkumbo huo wa kuelekea ligi ya Championship.
Matokeo ya mechi za mwisho za ligi hiyo…
Simba 2-0 JKT Tanzania
Coastal Union 0-0 KMC
Mashujaa FC 3-0 Dodoma Jiji
Ihefu 5-1 Mtibwa Sugar
Yanga 4-1 Prisons
Namungo FC 3-2 Tabora United
Geita Gold 0-2 Azam FC
Singida FG 2-3 Kagera Sugar
Soka Aziz Ki amfunika Fei Toto
Aziz Ki amfunika Fei Toto
Read also