Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag anamini bado anaweza kufukuzwa licha ya kuiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la FA.
Juzi Jumamosi, Ten Hag aliiwezesha Man United kubeba taji la FA baada ya kuwalaza mahasimu wao wa jiji la Manchester, Man City kwa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Wembley.
Ten Hag ambaye alianza mapumziko jana Jumapili hata hivyo yuko njia panda kuhusu majaliwa yake katika klabu hiyo na ana wasiwasi kwamba anaweza kutimuliwa baada ya vigogo wa klabu hiyo kufanya mapitio ya jinsi msimu ulivyokuwa katika vikao vyao.
Habari za ndani zinadai kwamba mapitio hayo yanatarajia kuanza wiki hii yakihusisha watu wazito ndani ya klabu hiyo na vikao vyao huenda vikachukua siku nne hadi kukamilika.
Uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya Ten Hag bado haujawekwa wazi lakini habari za ndani zinadai kwamba uamuzi huo utafikiwa mara baada ya vikao hivyo vitakavyofanya tathmini ya msimu mzima na kuamua kinachofuata.
Habari zaidi zinadai kwamba uamuzi wa mwisho utazingatia kiwango cha timu uwanjani lakini pia kama Ten Hag atafaa katika mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo ikiwamo kupunguziwa majukumu yakiwamo ya kusajili wachezaji.
Wakati vikao vikiendelea, makocha kadhaa wameanza kutajwa kuwa huenda mmoja wao akamrithi Ten Hag, makocha hao ni Mauricio Pochettino, Thomas Tuchel, Kieran McKenna na Thomas Frank ingawa bado habari ya makocha hao haijathibitishwa na yeyote ikiwamo mawakala wao.
Kimataifa Teg Hag ahofu kutimuliwa
Teg Hag ahofu kutimuliwa
Read also
