London, England
Man United hatimaye imebeba Kombe la FA kwa kuwanyuka mahasimu wao wa jiji la Manchester, Man City mabao 2-1 huku hatma ya kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag ikiendelea kuwa mjadala.
Ushindi wa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Wembley leo Jumamosi unatajwa kuwa huenda ukanusuru ajira ya kocha Erik ten Hag ambaye amekuwa na msimu mbaya.
Ten Hag anakuwa amebeba taji la pili tangu atue Man United miaka miwili iliyopita baada ya lile la Carabao na habari iliyopo sasa ni je atavumiliwa baada ya kubeba taji hilo au huu ni wakati sahihi wa kutimuliwa kwake?
Wako waliokuwa wakidai kwamba ushindi wa taji hilo utanusuru kibarua cha Ten Hag lakini hapo hapo kuna wanaodai kuwa, mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe alikuwa amejiandaa kumtimua kocha huyo bila kujali matokeo ya mechi ya leo.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola jana Ijumaa akiizungumzia mechi hiyo alisema kwamba iwapo Man United ingepoteza basi Ten Hag angekuwa katika matatizo.
Man United iliyoingia uwanjani ikiwa imepewa nafasi ndogo ya kushinda mechi hiyo, ilikuwa ya kwanza kuziona nyavu za Man City katika dakika ya 30 kwa bao lililofungwa na Alejadro Garnacho.
Dakika tisa baadaye, Kobbie Mainoo aliongeza bao la pili na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa 2-0 hali iliyotosha kuibua kila dalili za vigogo hao wa Manchester kubeba taji hilo.
Man City pamoja na kupambana kutaka kusawazisha mabao hayo, juhudi zao zilizaa matunda katika dakika ya 87 walipopata bao pekee la kufutia machozi lililofungwa na Jeremy Doku.
Kwa ushindi huo, Man United walau sasa imejihakikishia tiketi ya kucheza michuano ya Europa Ligi msimu ujao baada ya kukosa ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo inatajwa kuwa na hadhi ya klabu hiyo.
Kimataifa Man United yabeba mwali FA
Man United yabeba mwali FA
Read also