Munich, Ujerumani
Kocha wa Burnley, Vincent Kompany inadaiwa amefikia makubaliano ya awali na klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani ili awe kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi ya Thomas Tuchel aliyetimuliwa.
Habari za ndani zinadai kuwa kocha huyo aliyeipandisha Burnley Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita na kushuka nayo msimu huu, atasaini mkataba utakaofikia ukomo mwaka 2027.
Katika makubaliano hayo inadaiwa, Bayern watatakiwa kuwalipa Burnley zaidi ya Pauni milioni 10 kama malipo ya fidia kwa kuwa Kompany bado ana mkataba na Burnley.
Habari zaidi zinadai kwamba Kompany ambaye amepata nafasi hiyo baada ya makocha kadhaa kukataa ofa hiyo, akiwa Bayern hatokuwa pamoja na wasaidizi wake wote aliokuwa nao Burnley bali ataungana na baadhi yao.
Tangu Bayern itangaze kuachana na Tuchel, makocha kadhaa ambao wamekuwa wakitajwa kuwaniwa na timu hiyo wamekataa akiwamo Xabi Alonso wa Bayern Leverkusen.
Wengine waliokataa kuinoa timu hiyo ni Ralf Rangnick ambaye kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Austria na Julian Nagelsmann ambaye anainoa timu ya taifa ya Ujerumani.
Kompany, 38, beki wa zamani wa Man City na timu ya taifa ya Ubelgiji, inadaiwa pamoja na ubora wake katika kazi ya ukocha, pia anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kijerumani.
Kimataifa Kompany, Bayern mambo mazuri
Kompany, Bayern mambo mazuri
Read also
