Na mwandishi wetu
Yanga imeendeleza ubabe katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Dodoma Jiji FC mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa Jumatano hii jioni kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Wenyeji Dom Jiji licha ya kuwa nyumbani lakini walishindwa kuutumia vyema uwanja wao na kujikuta wakikumbana na fedheha hiyo kubwa wakati ligi ikielekea ukingoni.
Iliwachukua Yanga dakika 10 kuandika bao la kwanza ambalo lilifungwa na Clement Mzize kabla, Stephanie Aziz Ki hajaandika la pili dakika ya 45 na kuifanya Yanga iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mambo yalizidi kuwaendea vibaya Dom Jiji ambao walijikuta wakipachikwa bao la tatu dakika ya 51 mfungaji akiwa Aziz Ki kwa mara ya pili wakati bao la nne na la mwisho kwa Yanga lilifungwa na Maxi Nzengeli katika dakika ya 78.
Yanga tayari imeshafanikiwa kulibeba taji la ligi hiyo na inaendelea kucheza mechi zilizobaki kwa lengo la kuweka rekodi nzuri ya ushindi, imekusanya jumla ya pointi 74 katika mechi 28 na imebakiwa na mechi mbili za mwisho.
Kwa upande mwingine mabao mawili ya Aziz Ki yanakuwa muhimu kwake katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora akiwa anachuana kwa karibu na Feisal Salum au Fei Toto wa Azam FC.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Tabora United na Ihefu FC zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Ihefu likifungwa na Elvis Rupia na lile la Tabora likifungwa na Bikoko.
Soka Yanga yairarua Dom Jiji 4-0
Yanga yairarua Dom Jiji 4-0
Read also
