Na mwandishi wetu
Kuelekea mchezo wao wa kesho Jumanne dhidi ya Geita Gold, kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema maandalizi yamekamilika wakifahamu hautakuwa mchezo mwepesi.
Mgunda alisema kwamba pia wanawategemea mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuwapa nguvu katika mchezo huo muhimu kwao katika kutafuta nafasi ya pili.
Mgunda alisema hayo leo Jumatatu akieleza anafahamu timu hiyo ina wachezaji wazuri lakini pia ina kocha mzuri, Denis Kitambi hivyo wataingia wakifahamu uzito wa mchezo huo utakaopigwa kuanzia majira ya saa 1.00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dae es Salaam.
“Maandalizi ya kucheza mchezo wa kesho ambao ni mgumu, wenye ushindani, yanakwenda vizuri kwa hiyo tuko tayari kabisa kushindana katika mchezo mgumu wa kesho lakini mwisho wa yote kupata matokeo.
“Tunafahamu kabisa (Geita) wana mwalimu mzuri, wana vijana wazuri kwa hiyo kikubwa sisi tumejiandaa vizuri kucheza na timu nzuri. Katika wachezaji 11 watakaokuwa uwanjani, nina mchezaji wangu muhimu sana wa 12 ambaye ndiye sapoti yetu kubwa.
“Wakifanya sehemu yao wakiungana na wachezaji wa uwanjani basi naamini kabisa tulichokusudia kukipata au kukifikia kwa uwezo wa Mungu tutakifanikisha,” alisema Mgunda.
Naye kocha mkuu wa Geita, Denis Kitambi alisema pamoja ya kuwaheshimu Simba kutokana na wachezaji walionao wenye ubora katika kutumia nafasi lakini wamejiandaa kupambana nao.
Zaidi ya hilo Kitambi alisema kwamba wamejiandaa pia katika kutengeneza, kumiliki mpira na kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi wanazozipata ili wapate matokeo.
