London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ndoto zake za kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) kesho Jumapili zipo hai wakati huu akijiandaa kwa mechi ya mwisho iliyobeba hatma ya timu yake katika taji hilo.
Mabingwa watetezi, Man City wanashika usukani wa ligi hiyo wakiwazidi Arsenal walio nafasi ya pili kwa pointi mbili wakati Jumapili timu hizo kila moja itacheza mechi yake ya mwisho ya kufunga msimu.
Arsenal ili itwae taji hilo italazimika kushinda mechi hiyo dhidi ya Everton wakati huo huo ikiombea mabingwa watetezi Man City wapoteze au walau watoke sare mechi yao dhidi ya West Ham.
“Tulitaka kuwa katika nafasi hii, tumeshinda yote hadi kufikia hapa katika siku nzuri mbele ya watu wetu hapo Jumapili tukiwa na matumaini katika fursa hii kubwa kwamba tutabeba taji mwisho wa mechi hii,” alisema Arteta.
“Tuna uwezekano wa kuifurahia siku hii nzuri ya Jumapili, siku ambayo ndoto zetu bado zipo hai na bado tunaamini inawezekana, haya ndiyo mambo ya soka,” alisema Arteta.
Arteta anaelewa Man City ndiyo iliyo juu katika mbio za kulisaka taji hilo lakini ameamua kuweka nguvu na umakini katika mechi na Everton akiamini lolote linaweza kutokea katika mechi ya Man City na West Ham.
Artete ambaye amewahi kuwa mchezaji Arsenal hakuwahi kulibeba taji la EPL wakati huo na sasa anaamini litakuwa jambo kubwa kufanya hivyo na hiyo ni moja ya ndoto zake.
Mara ya mwisho Arsenal kubeba taji la EPL ilikuwa msimu wa 2003-04 wakati Man City inawania kuweka rekodi ya kulibeba taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.
