Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda amesema wakijipanga sawasawa wataondoka na pointi zote tisa katika mechi tatu zilizobaki za Ligi Kuu NBC kwa kuwa mechi zote hizo watazicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Mgunda alizungumza hayo baada ya jana Ijumaa kufanikiwa kuifunga Dodoma Jiji bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kuwa sawa na Azam FC kwa kufikisha pointi 60.
Azam hata hivyo bado inashikilia nafasi ya pili ikiwa juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga ingawa timu zote hizo kila moja imecheza mechi 27.
“Tumemaliza salama mechi za ugenini na sasa zimesalia za nyumbani tu, ni kweli ugenini ugumu unakuwepo na nyumbani inakuwa na nafuu yake lakini kikubwa ni kwamba tuko nyumbani.
“Tunapata muda wa kupumzika, yaani ile kuzunguka inakuwa haipo sababu hatusafiri tena, kwa hiyo naamini tukijipanga sawa sawa tutapata matokeo yaliyo mazuri katika mechi hizi,” alisema Mgunda.
Kuhusu mechi yao na Dodoma, Mgunda alisema waliingia na mpango mkakati wa kutafuta ushindi mapema maana walishafahamu ubora na udhaifu wa Dodoma na hawakutaka mpaka timu zizoeane kwa kuhofia mambo kuwa magumu zaidi.
Alisema kutokana na malengo waliyokuwa nayo hatimaye walifanikiwa kuandika bao hilo pekee dakika ya saba kupitia kwa Freddy Koublan na kuwapa pointi tatu muhimu.
Katika mechi tatu zilizosalia ambazo zitachezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Simba wataumana na Geita Gold Mei 21 kabla ya Mei 25 kuvaana na KMC kisha kufunga dimba na JKT Tanzania Mei 28, mwaka huu.
