London, England
Klabu ya Wolverhampton Wanderers imeanzisha kampeni ya kuachana na matumizi ya VAR katika Ligi Kuu England (EPL) ambapo klabu 20 za ligi hiyo zitapiga kura mwezi ujao kupitisha uamuzi huo.
Katika mpango huo, Wolves itahitaji kuungwa mkono na klabu nyingine 13 kwenye mkutano mkuu ambao utafanyika Juni 6 mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine utahusika kupitisha azimio hilo.
Uamuzi huo azma yake ni kuhakikisha matumizi ya VAR yanaachwa mara moja katika mechi zote za EPL lakini klabu pia zimepewa nafasi ya kuwasilisha hoja kinzani katika mkutano huo.
Taarifa ya Wolves iliyopatikana Jumatano ilieleza, “Hakuna suala la kulaumu, sote tunatafuta uamuzi ulio bora kwa ajili ya soka na wadau wake ambao wamefanya bidii kubwa kuanzisha teknolojia ambayo ilitakiwa iwe na mafanikio.”
“Hata hivyo baada ya misimu mitano ya VAR katika ligi kuu, tunadhani huu ni wakati wa kufanya mjadala wa kina kuhusu mustakabali wa jambo hili.
“Msimamo wetu ni kwamba madhara ambayo yanajitokeza kwa faida ndogo ya kutafuta usahihi ni makubwa na yenye sintofahamu hasa katika suala zima la kuinua ari ya soka hivyo tunataka tuondoe teknolojia hii kuanzia msimu wa 2024-25 na kuendelea,” ilieleza taarifa hiyo.
Miongoni mwa malalamiko ambayo yameainishwa na Wolves kuhusu VAR ni kuwachanganya mashabiki na kuibua utata viwanjani kutokana na muda ambao unatumika kuangalia VAR hadi kupata jibu.
Jingine ni hali ya furaha wanayokuwa nayo mashabiki baada ya kufungwa goli na hamasa inayokuwa kwenye soka vyote hivyo kuvurugwa.
Mashabiki kuzomea na kupinga matumizi ya VAR katika mechi ya ligi kuu ikiwamo kuukataa hadi wimbo wa ligi hiyo.
Wolves pia wanadai licha ya kuwapo kwa VAR lakini bado kumekuwa na makosa na kuwafanya mashabiki kutokubali makosa ya kibinadamu baada ya kuirudia mechi mara kadhaa hali ambayo pia inaathiri uwezo wa kujiamini wa waamuzi.