Na mwandishi wetu
Mechi ya Ligi Kuu NBC kati ya Simba na Dodoma Jiji iliyopangwa kuchezwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro imesogezwa mbele kwa siku moja na sasa itapigwa Ijumaa ya Mei 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), mechi hiyo imelazimika kusogezwa mbele kwa siku moja zaidi ili kuipa nafasi ya kikanuni Dodoma Jiji ya kucheza mechi nyingine ya kimashindano baada ya saa 72.
Akizungumzia mchezo huo, kaimu kocha mkuu Simba, Juma Mgunda alisema kwamba maandalizi yanaendelea vizuri ili kurekebisha kikamilifu makosa yaliyotokea katika mchezo wao uliopita.
Katika mchezo uliopita, Simba au Wekundu wa Msimbazi walikubali kuvutwa shati na Kagera Sugar baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Mgunda alisema bado wanaendelea kupambana kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zao nne zilizosalia kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la ligi hiyo msimu huu.
Simba inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa inapambana kujinasua ili imalize katika nafasi ya pili ya ligi hiyo ikipambana na Azam FC na hiyo ni baada ya kuukosa ubingwa ambao tayari umebebwa na mahasimu wao, Yanga.
Soka Mechi ya Simba, Dom Jiji sasa Mei 17
Mechi ya Simba, Dom Jiji sasa Mei 17
Read also