Na mwandishi wetu
Azam FC haifurahishwi na namna inavyotambulishwa kama timu inayopambania nafasi ya pili na kuondolewa kwenye mbio za ubingwa msimu huu, kitu ambacho wanaamini si sahihi na lolote linawezekana ikiwamo kubeba taji la ubingwa.
Kauli hiyo imetolewa na meneja habai na mawasiliano wa Azam, Thabiti Zakaria (pichani) akianza kwa kufafanua kuwa nafasi ya pili tayari wao ndio wanaimiliki kwa sasa.
Zakaria hata hivyo amesema kwamba wala hawaipiganii nafasi hiyo kama inavyoelezwa, badala yake wao wanatazamia wanaifikiaje nafasi ya kwanza inayoshikiliwa na Yanga SC.
“Huwa sipendi sana kuzungumzia kuhusu kushindana nafasi ya pili, sisi hatushindanii nafasi ya pili, sisi tupo nafasi ya pili maana hiyo nafasi tayari tunayo mfukoni, maana yake tunashindania nafasi ya kwanza, tunaangalia juu zaidi na sio tena hapa ambapo tunapo.
“Wanaopaswa kugombania nafasi ya pili ni hao walioko chini yetu ndio wanaoshindania, walioko huko nyuma ndio wanashindania nafasi hiyo sababu mpaka sasa hivi ligi haijaisha na bado bingwa hajapatikana,” alisema Zakaria.
“Sasa ni kwa nini Azam iwe inawekwa nafasi ya pili tu wakati wa juu anaweza akapoteza maana huu ni mchezo kwa hiyo nafasi hiyo ipo msiikatie tamaa kabisa, msifunge milango katika hilo” alisema Zakaria.
Ikiwa imesalia michezo takriban mitatu mpaka minne kabla ya kufungwa kwa Ligi Kuu NBC msimu huu, Yanga inaongoza kileleni kwa pointi 68 kabla ya mchezo wao wa Jumatatu dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam iko nafasi ya pili kwa pointi 60 na Simba inashika nafasi ya tatu kwa pointi 57.
